KANUNI ZA KILIMO HAI
Maana ya kilimohai.
Kilimohai kinahusisha shughuli zote zinazofanyika katika uzalishaji wa bidhaa na mazao ili kukidhi mahitaji yetu kwa kuzingatia kanuni za msingi na viwango vilivyoanishwa.
IFOAM
inatafsiri kilimohai kuwa ni "mfumo wa uzalishaji unaojali, zingatia ma kuendeleza rutuba katika udongo, ikolojia pamoja na watu. Unategemea mchakato wa kiikolojia, nioanuai na hali ya kimazingira kuliko kutegemea matumizi ya pembejeo zenye kuleta madhara. Kilimohai kinahusisha ujuzi na maarifa ya asili, ubunifu na utafiti wa kisayansi katika kuinua uzalishaji na kuhimiza utunzaji mazingira, kuhuisha usawa na haki na kuboresha hali ya maisha.
FAO
Inatafsiri kilimohai kuwa ni sehemu ya kilimo endelkevu kinachohusisha mbinu rafiki zenye kuhifadhi mazingira na zinazowezesha uzalishaji wa mazao na mifugo pasipo kusababisha madhara au uharibifu katika ikolojia ya shamba, rutuba ya udongo, uwepo wa maji, bayoanuai na mali asili zinazozunguka shamba. Dhana ya kilimo endelevu inaazingata kizazi cha sasa na vijavyo kwa kuhifadhi na kuboresha mali asili badala ya kuharibu na kumalizika.
CODEX ALIMENTARIUS COMMISSION
Pia inatafsiri " Kilimohai ni miongoni mwa njia nyingi zinazosaidia hifadhimazingira. Mfumo wa kilimohai umeweka kanuni na viwango mahususi vinavopaswa kuzingatiwa wakati wa uzalishaji kwa lengo la kuhusisha ikolojia na uendelevu wa ikolojia na uendelevu wa mazingira na jamii.
Neno kilimohain au "Organic" linatumika kutambulisha bidhaa iliyozalishwa kwa kuzingatia viwango na kanuni za kilimohai na kupata utibitisho wa hati na lama kutoka kwa mamlamka ya uthibiti ubora na viwango.
Utangulizi wa kanuni za kilimohai
Kanuni ndio msingi wa kilimo hai na mchango unaoweza kuifanya dunia kuboresha kilimo duniani kwa ujumla. Kilimo ni moja ya shughuli muhimu zinazofanywa na binadamu kwa ajili ya kupata mahitaji ya kila siku ili kujikimu. Hata historia, mila na thamani za watu katika jamii zinaambatana na maendeleo katika kilimo.
Kanuni zinazotumika katika kilimo kwa ujumla zinahusisha mtazamo wa watu juu ya udongo, maji,mimea na wanyama katika kuzalisha, kuandaa na kusambaza chakula na bidhaa nyinginezo.Zinaonesha namna watu wanavyo ona uhai na mandhari ya ardhi, mahusiano miongoni mwao na mwelekeo wa matumaini kuhusu vizazi vijavyo. Kanuni za kilimo hai zinalenga kuhuisha vuguvugu la kilimo hicho katika nyanja zote. Zinatoa mwongozo kwa "IFOAM" katika kuweka vipaumbele juu ya maendeleo, mipango na viwango. Isitoshe, kanuni hizi zinawakilisha mtazamo wake kidunia.
Kanuni za msingi wa kilimo hai
Kuna kanuni nne za msingi wa kilimo kama zilivyofafanuliwa na IFOAM
i. Kanuni ya Mazingira
ii. Kanuni ya Afya
iii. Kanuni ya Haki na Usawa
iv. Kanuni ya Huduma
Kanuni hizi zimefungamana na kwa ujumla wake zinabeba kivitendo matarajio ya kilimo hai japo kila moja ya kanuni ina maelezo yake ya ufafanuzi.
Kanuni ya mazingira
Kilimo hai sharti kisimamie na kujaliuhai wa mfumo wa mazingira na mzunguko asilia, kuishi na kufanya kazi sanjari na kuchangia katika kufanya kilimo kiwe endelevu.
Kanuni hii huweka msingi wa kilimo hai katika kuhusisha na kuhifadhi mazingira. Inasisitiza juu ya uzalishaji yanayojali na kutegemea mchakato endelevu wa kimazingira. Hali iliyobora na ustawi hupatikana kwa kutegemea mazingira ya uzalishaji unaojali uhai wa viumbe wengine. Kwa mfano uzalishaji wa mazao unapaswa kuzingatia uhai wa udongo; ufugaji wa wanyama unaozingatia mfumo wa kimazingira.
Pamoja na kuwa kilimo hai kinaendana na mazingira ya kawaida na tamaduni za mahali popote duniani kwa kuzingatia kanuni za msingi, matumizi ya pembejeo sanisia/ kemikali ni sharti yapungue, kuongeza uwajibikaji katika kutumia rasilimali na maliasili, pale inapowekana kurejeshwa upya na kutumika tena. Kuwa na usimamizi sahihi wa malighafi na nishati ili kuboresha mazingira na kuhifadhi maliasili na rasilimali.
Kilimo hai lazoma kifanikishe uwiano wa kimazingira kwa kubuni na kuhimiza mfumo wa uzalishaji unaoweka mazingira bora kwa makazi na kutunza uithi wa kimaumbile na kilimo. Wanaozalisha, kusindika, kuuza au kutuma bidhaa za kilimo hai wanastahili kulinda uwiano huu kwa manufaa ya mazingira kwa ujumla ikiwa ni pamoja na hali hewa, viumbe, bayoanuai, hewa na maji.
Kanuni ya Afya
Kilimo hai sharti kiwe endelevu na kudumisha rutuba ya udongo, kiboreshe afya ya mimea, wanyama, binadamu katika sayari hii kama kitu kimoja. Kanuni hii inaashiria kuwa afya ya watu au jamii haiwezi kamwe kutengwa na afya ya kimazingira- ardhi yenye afya huzalisha mazao yenye ubora kwa afya na uhai wa binadamu na wanyama.
Afya ni mfumo wa uhai na taratibu za maisha ikimaanisha kutokuwepo magonjwa, kujali na kutunza mwili, akili, ustawi wa jamii, mazingira bora na mazuri kuishi. Uwezo wa kujikinga, kushiriki katika uumbaji na kujijali na tabia ya msingi na muhimu kwa afya bora
Jukumu la kilimo hai- iwe katika ulimaji, usindikajai, usambazaji,
Usambazaji au ulaji- ni kuendeleza na uboresha afya na uhai, mfumo wa mazingira na viumbe aina zote kuanzia kwenye udongo hadi binadamu.
Kwa hakika, kilimo hai kinalenga katika uzalishaji wa chakula kinachokidhi viwango vya ubora na usalama wa hali ya juu ili kuchangia katika kujikinga na kujenga siha nzuri.
kwa kuzingatia afya, usalama na uhai, kanuni za kilimo hai zinazuia matumizi holela ya mbolea, madawa ya wadudu au magonjwa ya mifugo na viatilifu au vinasaba vinavyoongezwa katika hifadhi ya vyakula ambavyo vinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa mlaji au mtumiaji.
Kanuni ya haki
Kilimo hai sharti kizingatie msingi wa mahusiano yatakayohakikisha usawa katika mazingira na fursa ya kuishi. Usawa unaojali na kuzingatia heshima, haki na kujituma kwa kila mmoja wetu na mahusiano ya viumbe hai kwa ujumla.
Kanuni hii inasisistiza kuwa wale wote wanaojihusisha na kilimo hai lazima wazingatie mahusiano yenye usawa katika ngazi zote bila upendeleo, iwe kwa wazalishaji, walaji, wasindikaji, wafanyakazi, wafanyabiashara na wasambazaji ili kuboesha mazingira na kuhifadhi maliasili na rasilimali.
Kilimo hai lazima kifanikishe uwiano na urari wa kimazingira kwa kubuni na kuhimiza mfumo na kutunza rasilimali asilia na ukuaji wa kilimo.
Wote wanaozalisha , wanaosindika, wanaouza au kununua, kula na kutumia bidhaa za kilimo hai wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kukinga na kuzuia uharibifu wa mfumo mzima wa mazingira unayojumuisha hali ya hewa, viumbe, bayoanuai, hewa na maji.
Kilimo hai kinapaswa kuwapatia maisha bora na mazuri wale wote wanaojihusisha nacho na kuchangia katika uhakika wa chakula na kupunguza umaskini.
Malengo ya kilimo hai ni kuzalisha chakula na bidhaa za kutosha kwa kuzingatia viwango vya ubora. Kanuni inasisitiza kuwa wanyama lazima wapatiwe fursa na hali ya kimazingira inayoendana na maumbile, tabia zao za asili na hali bora.
Rasilimali za asili na za kimazingira zinazotumika katika uzalishaji au matumizi mengine ni lazima zisimamiwe vema na matumizi hayo yakubalike kuwa tija kwa jamii na ikolojia ya mazingira kwa kujali haki na urithi wa vizazi vijavyo. Mfumo wa uzalishaji, usambazaji na biashara wenye uwazi, haki na unaowajibika kwa mazingira na jamii unahitajika ili kujenga usawa na haki.
Kanuni ya uangalizi
Kilimo hai lazima kiweke tahadhari na uwajibikaji unaoweka kinga kwa afya na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo pamoja na kujali mazingira endelevu.
Mfumo wa kilimo hai unapaswa kubadilika ili kuendana na matakwa ya hali ya ndani au nje ya mazingira husika. Wanaojihusisha na kilimo hiki wanapaswa kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji, pasipo kuleta athari za kiafya na ustawi kwa kufanyika tathimini na uchambuzi wa teknolojia mpya na zilizopo.
Kwa kuwa hakujafikiwa muafaka wa uelewa juu ya mfumo wa kimazingira na kilimo, tahadhari ya uangalizi lazima ichukuliwe. Kanuni hii inaweka tahadhari na wajibu muhimu wakati wa kuchagua teknolojia za kilimo hai kwa kuzingatia maendeleo na mazingira endelevu.
Inatambua kuwa sayansi ni muhimu kwa kilimo kwa kilimo hai ili kiwe salama na bora kwa mazingira, binadamu,viumbe n.k. Hata hivyo, maarifa ya kisayansi pekee hayatoshi, ujuzi na maarifa ya asili, uzoefu, hekima, busara na ubunifu uliojengeka kwa vizazi kadhaa unahitajika kutoa suluhisho na ufumbuzi wa matatizo ya mazingira na uzalishaji. Kilimo hai lazima kizuie athari kwa kubuni na kutumia teknolojia sahihi. Pia kuzikataa zile ambazo sio endelevu na ambazo athari zake hazijafahamika bayana kama vile viini tete au GMO
Maamuzi ya teknolojia na pembejeo gani zitumike katika kilimo lazima yazingatie amali na mahitaji ya wote waoweza kuathirika, hivyo ni muhimu wahusishwe katika mchakato ulio wazi na shirikishi wakati wa kuchambua na kuchagua teknolojia.