MCHANGO WA WANAWAKE KATIKA UZALISHAJI WA MAZAO YA CHAKULA

Share:


Nchini Tanzania sehemu kubwa sana ya chakula tunachokula huzalishwa na wakulima wadogo ambao wastani wa mashamba yao ni kati ya nusu hekta na hekta mbili na nusu. Siyo rahisi kutoa tafsiri kamilifu ya "mkulima mdogo". Yatosha kusema kwamba ni mtu ambaye yeye na familia yake hustawisha mazao ili wajikimu. Mara nyingi hufanya kazi zingine nje ya kilimo za kuwaletea kipato.

Wanawake ndani ya familia ndio wazalishaji wakuu wa mazao ya kilimo, hasa ya chakula. Huchukua masaa mengi mchana kutwa shambani hadi nyumbani wakishughulika na kulima, kupanda, kupalilia, kuvuna, kusindika, na kupeleka sokoni. Majukumu mengine ni kutunza mifugo na wanafamilia wasiojiweza, kutafuta kuni na kuchota maji na kupika.

Kwa hiyo, mchango wa wanawake katika kuhakikishia familia ina chakula cha kutosheleza mahitaji yao ni mkubwa mno. " Uhakika wa chakula" (Food Security) maana yake ni kupata chakula chenye lishe inayokubalika. Hali hii hufikiwa endapo watu wote kwenye eneo fulani wanapata cha kuwapatia nguvu ya kufanya kazi zao, pia kuwa na afya nzuri. Kwenye ngazi ya taifa, uhakika wa chakula unahusishwa na uwezo wa taifa wa kutosheleza mahitaji ya jumla ya raia wake kutokana na uzalishaji wa ndani au kununua kutoka nje.

Kwenye kaya, uhakika wa chakula haukomei kwenye kuzalisha tu. Pia Unamaanisha kupata ziada ya kuuza au kustawisha mazao mengine ya kibiashara ili kutosheleza mahitaji mengine muhimu ya familia. Kwa kuwa wanawake ndio wachangiaji namba moja, tunapozungumzia suala la uhakika wa chakula, budi tuzungumzie uwezeshaji wa kikundi hiki. Kwa ukweli huu basi, kuimarisha hali ya uhakika wa chakula inaamaanisha kuwezesha wanawake wakulima.

Mahitaji ya wanawake wakulima ni mengi, yakiwemo fursa ya kuchangia mawazo wakati wa kupanga nini kifanyike na jinsi gani kifanyike, umiliki wa rasilimali hasa ardhi, ushariki wao katika kutunga sera na kufanya maamuzi yanayohusu utendaji kazi. Katika masuala haya, mara nyingi wanawake hepewa fursa ndogo ya kuhusishwa, au hawahusishwi kabisa. Mbaya zaidi, ardhi wanayoitumia hawaimiliki, ni mali ya waume zao au watoto wao wa kiume. Kwani tamaduni karibu zote za Kiafrika, ardhi hurithishwa kwa vizazi vya kiume.

Mbaya zaidi, uamuzi kuhusu kwa vipi wanawake wanaweza kupata ardhi, na kwa vipi waitumie, maranyingi unafanywa na wanaume. Ardhi nzuri kwa kilimo hutumiwa na wanaume  kustawisha mazao ya kibiashara, ardhi duni huwaachia akina mama kwa ajili ya kuzalisha mazao ya chakula. Pamoja na mchango wao, wanawake hawapewi nafasi kubwa ya kuhudhuria mafunzo kuhusu shughuli wazifanyazo. Aidha, mfumo wa maunzo ya kilimo uliopo  unapendelea wanaume kwa kulenga zaidi uendelezaji wa kilimo cha mazao ya biashara, ambayo kwa sehemu kubwa humilikiwa na akina baba.

Mara nyingi wanawake wakulima hutenga kiasi fulani cha mavuno kwa ajili ya kuuza ili wakidhi mahitaji mengine ya kifamilia. Ni makini sana katika kutunza familia. Hata hivyo, wakati mwingine wakulima huingia kwenye mtego wa kuuza kiasi kikubwa cha mavuno na kubakisha kisichowatosheleza  hadi msimu wa mavuno mengine. Tatizo lingine ni hifadhi mbaya ya akiba. Mazao yasipohifadhiwa vizuri kuharibika kwa unyevu, panya, na wadudu. Katika hali ya kawaida, uharibifu huo hufikia asilia 30 au zaidi.

Wanawake wana majukumu mengi ya kifamilia. Ikiwa ni pamoja na kulea watoto, kutunza vikongwe, na kuuguza wagonjwa. Haya ni baadhi ya majukumu amabayo mara nyingi hukwepwa na wanaume. Tukiri kwamba majukumu ya ziada hayawapi muda wa kutosha wa kushughulika na kilimo, hivyo kufifisha uwezo wao wa kuzalisha zaidi.

Maendeleo katika sekta ya kilimo nchini Tanzania yatakwama iwapo changamoto zinazokabili wanawake wakulima hazitatafutiwa ufumbuzi wa kudumu. Kwa hiyo, programu na miradi inayohusiana na kilimo sharti itilie maanani masuala ya jinsia, uwezeshaji wa wanawake, na mgawano sawa wa mapato.