MUENDELEZO: MADHARA YA MAZAO YALIYOBADILISHWA VINASABA KWA JAMII

Share:

Inaendelea ilipoishia

Nguvu Kazi ya Vijijini
Mbegu nyingi zilizobadilishwa vinasaba zimetengenezwa ili kukidhi mahitaji na mazingira ya wakulima katika nchi zilizoendelea ambapo kilimo chao kinahusisha mashamba makubwa. Kilimo cha aina hii ambapo upatikanaji wa nguvu kazi ni changamoto ni tofauti na kile cha mkulima mdogo cha ngazi ya kaya ambapo nguvu kazi kwa kiasi kikubwa inapatikana kwa gharama nafuu. Kwa mfano, mazao yaliyobadilishwa vinasaba ili kutoa ukinzani dhidi ya sumu ya magugu huondoa hitaji la nguvu kazi ya kupalilia na kuandaa shamba ambapo inaathiri ongezeko la mahitaji ya nguvu kazi. Nguvu kazi kidogo inayohitajika kwa ajili ya kilimo inaathiri ajira kwa wale wanaotegemea kufanya kazi za vibarua mashambani ili kujiongezea kipato.

Biashara
Mojawapo ya jambo muhimu la kuliangalia katika biashara ni uwezo wa nchi zinazoendelea, kama Tanzania, katika kushindana na nchi zilizoendelea, kama Tanzania, katika kushindana na nchi zilizoendelea katika soko la kimataifa pindi zitakapojihushisha kikamilifu na kilimo cha mazao yaliyobadilishwa vinasaba. Ili kutoa ushindani huo itabidi nchi zinazoendelea kukidhi viwango vya ubora wa hali ya juu vya bidhaa vilivyowekwa kwenye soko hilo. Bidhaa kutoka katika nchi zinazoendelea zinaweza kushindwa kuingia katika soko la kimatifa kwa kutokidhi viwango vya ubora.

Kuishi pamoja na kuchafuliwa
Mazao yaliyobadilishwa vinasaba yanapochanganywa na mazao mengine kunahatari ya kuhamisha chavua hasa kwa mazao ambayo yana uchavushaji mtambuka kama vile mahindi. Wakulima wanaofuata mbinu za kilimo hai wana hatari ya mazao yao kuchafuliwa na yale yaliyobadilishwa vinasaba kupitia chavua. Hii ni kwasababu chavua zina uwezo wa kusafiri umbali mrefu kwa kusaidiwa na upepo au wadudu. uchafuzi huu unaweza kutokea zaidi pale ambapo wakulima wana mashamba madogo na umbali toka shamba moja hadi jingine ni mfupi. Uchafuzi unaofanywa na mazao yaliyobadilishwa vinasaba kwa mazao mengine na magugu ni tishio kwa bioanuai na kwa uhakika wa chakula. Uchafuzi unaweza kutokea wakati wa kusafirisha na kusindika mazao.

Kilimo hai
Mazao yaliyobadilishwa vinasaba ni tishio kwa maendeleo ya kilimo hai. Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye wakulima wengi waliohakikiwa kulima mazao kwa kufuatakanuni za kilimo hai. Kwa mujibu wa IFOAM 2014 Tanzania inashikilia nafasi ya nne duniani kwa kuwa na idadi ya wakulima wapatao 148.610 waliohakikiwa kuzalisha mazao ya kilimo hai. Baadhi ya mazao yanayozalishwa ni pamoja na viungo, kahawa, pamba  na kakao ambayo  huuzwa katika soko la nje, Kanuni za uhakiki za bidhaa za kilimo hai haziruhusu mazao yaliyobadilishwa vinasaba. Hivyo uchafuzi wa mazao ya kilimo hai unaofanywa na mazao yaliyobaadilishwa vinasaba huharibu soko la bidhaa hizo ambalo linazidi kuongezeka duniani.

Uhakiki wa chakula
Katika nchi zinazoendelea kilimo ndicho kinaihakikishia kaya kujikimu na upatikanaji wa chakula na ziada ya kuuza katika soko la ndani. Kiasi kikubwa cha mazao yaliyobadilishwa vinasaba ambayo hulimwa sehemu mbalimbali duniani, yanakuwa si kwa ajili ya chakula cha binadamu bali kwa ajili ya mifugo na utengenezaji wa mafuta ya kuendeshea mitambo.  Mfano, katika nchi ya Marekani, mahindi yaliyobadilishwa vinasaba yanachangia chini ya 15% na soya chini ya 5% (GM Watch, 2009). Ulimaji wa mazao yaliyobadilishwa vinasaba katika nchi zinazoendelea utageuza ardhi ambayo hutumika  kwa ajili ya kuzalisha mazao ya chakula ili kuzalisha bidhaa za mazao kwa ajili ya matumizi ya viwandani na usafirishaji nje ya nchi na hivyo kutishia uhakika wa chakula

Itaendelea........................