Na Constantine Akitanda, aliyekuwa Dodoma
WAZIRI Mkuu Mstaafu wa awamu ya nne Mh. Mizengo Peter Pinda amesifu
jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Uendelezaji Kilimohai Tanzania
(TOAM), kwa kile alichokiita kuwa jitihada za uendelezaji kilimohai
kwa sasa ni jambo lisiloepukika.
Mh. Pinda ameyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma
baada ya kutembelewa nyumbani kwake Zuzu na Mkurugenzi Mkuu wa TOAM
nchini ambaye pia ni Rais wa Mtandao wa Kilimohai Barani Afrkika, Bw.
Jordan Gama.
Nakushukuru ndugu Gama kwa kunitembelea hapa kijijini kwetu , mimi
nimeweka makazi hapa, na hakika naendesha kilimo kwa asilimia kubwa
kufuata mfumo wa kilimohai, nafanya hivi kwasababu naelewa umuhimu wa
kupata chakula salama lakini vilevile umuhimu wa kuilinda ardhi na
viumbe vilivyomo ndani yake.
Niliamua tangu awali kujikita katika kilimo cha namna hii, na kwa
kweli ninakifurahia, kwa kuwa natumia mbolea ya samadi itokanayo na
wanyama ninaowakuza hapa hapa shambani, awali nilikuwa napata kwa
wafugaji ambao baadaye walianza kuuza kwa gharama ya TZS 35,000 kwa
lori, lakini kubwa zaidi ni kwamba uzalishaji kwa kutumia mbolea ya
samadi hufanya mazao yahimili hali ya ukame na kupata mavuno kuliko
mazao ya shamba lisilotumia mbolea hii, alisema Waziri Mkuu Mstaafu.
Mh. Pinda ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa umma na
viongozi mbalimbali nchini na dunia kwa ujumla kujenga utamaduni wa
kujiwekeza kwenye kilimo, kwa kuwa kilimo kimekuwa na tabia ya
kumlinda na kumsitiri yeyote yule mwenye malengo ya kuishi maisha ya
kipato cha kati na hata ya kiwango cha juu baada ya kustaafu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TOAM, Bw. Gama, alimhakikishia
Waziri Mkuu Mstaafu kuwa amevutiwa kufanya ziara katika shamba hilo
baada ya kuona jitihada zake kubwa katika kujaribu kulima kwa mfumo
wa kilimohai kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
“Mh. Waziri Mkuu mstaafu, nitumie fursa hii kukupongeza kwa uamuzi
wako wa kuwa mfano mwema kwa wastaafu na Watanzania kwa ujumla, sisi
TOAM, tutashirikiana nawe bega kwa bega katika kuhamasisha na
kuelimisha jamii kuiga kilimo cha aina hii unachokiendesha, bila
shaka ziara hii hapa leo itafungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika
jitihada zako za kuendeleza kilimohai,” alisema Gama.
“Tumejionea bayana kuwa eneo hili ni kame sana, na kwamba baadhi ya
mazao pamoja na jitihada zako za kufanya umwagiliaji yanaweza
yasifanye vyema sana, tunaomba uturuhusu tulete mimea itakayosaidia
kuongeza rutuba na kutunza unyevu katika ardhi ili mazao yaweze kukua
vema, kupitia kazi yako hii ya kilimo, tunaona fursa kwetu ya kufanya
shamba hili kuwa kitivo cha mafunzo kwa wakulima wa kada zote,”
alisisitiza Gama.
Gama akaongeza kuwa kwa sasa sehemu kubwa ya dunia mwamko wa
kilimohai umekuwa mkubwa sana, na kwamba nchi za Ulaya zenye uchumi
mkubwa kama Ujerumani kasi ya kubadili mashamba yao kutoka kilimo cha
kutumia kemikali inaongezeka na kuwa ya kilimohai, lakini kubwa zaidi
ni kwamba katika nchi hiyo kilimo cha kutumia pembejeo
zilizobadilishwa vinasaba (GMO) hakijaruhusiwa na mamlaka zote za
kiserikali.
Akizungumzia kuhusu GMO, Mh. Pinda alisema serikali wakati akiwa
madarakani iliruhusu utafiti wa GMO ili kujiridhisha pasipo shaka
kuhusu usalama na manufaa ya teknolojia hiyo kwani imekuwa na mtazamo
uliogawanyika kote duniani na nchi mbalimbali kuchukua maamuzi ya
kuiruhusu au kuizuia ili kujiridhisha na hoja zinazokinzana.
Wakati huo huo, barani Afrika, nchi ya Ethiopia imetajwa kuwa
ni mojawapo ya nchi zinazopiga hatua kwa kasi zaidi kwa ongezeko la
wazalishaji wa bidhaa za kilimo hai ikifuatiwa na Tanzania.
Miongoni mwa majukumu ya TOAM ni kuwaunganisha wakulima na masoko,
ili kuongeza tija katika uzalishaji, miongoni mwa taasisi
zinazozalisha kwa mfumo wa kilimohai nchini ni pamoja na Vyama vya
Ushirirka vya Kagera (KCU); Kilimanjaro (KNCU) na kampuni binafsi
(BIORE) zinazofanya biashara na uzalishaji wa bidhaa/mazao kwa
kuzingatia viwango na mfumo wa kilimohai. Wengine ni vikundi na
mkulima mmoja mmoja.
Taasisi ya uendelezaji kilimohai nchini yaani Tanzania Organic
Agriculture Movement (TOAM), ni taasisi mwamvuli, ambayo inaunganisha
wadau mbalimbali wa kilimohai, wakiwemo, wazalishaji, watafiti na
waelimishaji, wauzaji, makampuni na asasi za kiraia pamoja na vikundi
vinavyozalisha mazao kwa mfumo wa kilimo hai.
Kwa sasa makao makuu ya kilimo hai barani Afrika yapo nchini
Tanzania, na Rais wa Kilimo Hai ni Mtanzania, na kwamba taasisi hii
inafanya kazi kwa karibu sana na serikali kupitia Wizara ya Kilimo,
sambamba na mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na kilimohai kama
International Forum for Organic Agriculture Movement (IFOAM), United
Nation Conference on Trade and Development (UNCTD) na African
Union Commission (AUC).