UZALISHAJI WA MBEGU BORA YA MBAAZI

Share:
Mbaazi ni zao ambalo ni jamii ya mikunde. Zao hili hustahimili ukame na huzalishwa kwenye maeneo mengi hapa nchini. Karibu mikoa yote Tanzania hulima mbaazi kama zao la chakula na biashara. Zao hili linastawi kwenye mwinuko wa mita 0- 2000 kutoka usawa wa bahari.

MAZINGIRA BORA
Hali ya hewa
Mbaazi hutaawi kwenye maeneo yenye kupata mvua za chini (mm 500) hadi zinazopata mvua za kutosha (mm 1500)
Aina ya Udongo
Mbaazi hustawi vizuri karibu katika aina zote za udongo wenye rutuba ya kutosha. Udongo usiotuamisha maji unapendekezwa katika uzalishaji wa zao hili.
SIFA YA SHAMBA
Historia ya shamba
Mzalishaji aepuke kuzalisha mbegu kwenye shamba ambalo msimu uliopita lilipandwa mbaazi, isipokuwa kama mbaazi zilikuwa za jamii (aina) ile ile na daraja la juu.
Utenganisho wa shamba
Shamba la mbaazi linatakiwa kutengwa kutoka shamba lingine la mbaazi kwa umbali wa mita 50.
Sifa za ziada katika uzalishaji wa mbegu
Mzalishaji anapaswa awe na utaratibu kwa kutopanda mfululizo zao hili katika shamba moja ili kuepuka magonjwa kama mnyauko wa mimea
UTAYARISHAJI WA SHAMBA
Shamba jipya
Shamba jipya lafaa kung'olewa visiki kabla ya kuanza kutifua ardhi
Shamba la zamani
Shamba la zamani linaweza kutifuliwa kwa kutumia aidha wanyama kazi, jembe la mkono au trekta. Hakikisha kwamba shamba limetifuliwa kina cha kutosha na mabonge yapigwe ili kupata udongo laini.

Chanzo cha mbegu
Mbegu zitakazotumika katika uzalishaji zisiwe chotara. Mkulima atumie mbegu ya daraja la msingi, au kuthibitishwa ama QDS 1. Mbegu ya msingi na iliyothibitishwa hupatikana katika mashamba ya wakala wa mbegu za kilimo (Agricultural Seed Agency-ASA). Vilevile mbegu za daraja la kuthibitishwa hupatikana katika makampuni ya mbegu, kupitia kwa wakala wao au maduka ya pembejeo.
Mkulima anaruhusiwa kutumia mbegu ya QDS 1 iliyopatikana kutoka kwa mkulima wa mbegu aliyesajiliwa na TOSCI, kama chanzo cha mbegu, lakini ajue ya kwamba, akishavuna haezi kuitumia kama mbegu tena. Aina ya mbegu zinazopendekezwa na wizara ya kilimo ni komboa, mali, tumia.
UPANDAJI
WAKATI WA KUPANDA
Mzalishaji anashauriwa kuzalisha mbegu wakati wa mvua za msimu. Mbaazi za muda mfupi hustawi zaidi ukanda wa chini na ni vyema zikapandwa mwishoni mwa mwezi wa Februai kwani hukomaa katika muda wa siku 120.
Mbaazi za muda mrefu hustawi vema kwenye ukanda wa kati na wa juu na huchukua muda wa siku 180 kukomaa. Aina hizi zipandwe mwezi Disemba na Januari.
Kiasi cha mbegu
Ili kupanda ekari moja unahitaji kilo 3 za mbegu ya muda mfupi na kilo 2 za mbegu ya muda mrefu.

NAFASI YA KUPANDA
Mbaazi za muda mfupi
Panda kwa umbali wa sentimita 50 kati ya mistari na sentimeta 20 kati ya mashina. Panda mbegu 2 kila shimo, mwishoni bakiza shina moja tu.
Mbaazi za muda mrefu
Panda kwa umbali wa sentimeta 180 kati ya mstari na sentimeta 50 kati ya mashina. Panda mbegu 2 na mwishoni bakiza mmea 1 kwa kila shina.

MATUMIZI YA MBOLEA
Mbaazi ikiwa ni zao jamii la mikunde hutengeneza mbolea ardhini, hata hivyo ni vyema mzalishaji arutubishe shamba lake ili kupata mavuno mengi. Tumia samadi iliyoboreshwa kama mbolea ya kupandia. Usitumie mbolea za kukuzia kwani mbaazi huwa zinajitengenezea zenyewe virutubisho vya kujikuzia.

KUSAJILI SHAMBA LA MBEGU
Mara baada ya kupanda, mzalishaji analazimika kusajili shamba lake katika Taaasisi ya udhibiti wa ubora wa mbegu (TOSCI) aidha katika kituo cha Mororgoro, Njombe au Arusha au sehemu nyingine ambazo taasisi hiyo ina ofisi katika muda usiozidi siku 30 ili kutoa nafasi wakaguzi hao kupanga utaratibu wa ukaguzi.

PALIZI
Hakikisha shamba linakuwa safi kwa kupalilia mara kwa mara katika wiki 6 za mwanzo. Baada ya hapo palilia tu inapobidi kufanya hivyo.

KUNG'OA MIMEA ISIYOFAA NA YENYE UGONJWA
Toa mimea yote ambayo haifanani na mimea husika, pia ondoa mimea yote yenye ugonjwa

UDHIBITI WA MAGONJWA NA WADUDU WAHAIBIFU
Magonjwa
Mbaazi hushambuliwa na magonjwa ya mnyauko, mzalishaji aonapo mmea wenye dalili hizi aung'oe na kutupa nje ya shamba.
Uzuiaji Wadudu
Mbaazi za muda mfupi, hushambuliwa sana na wadudu, Nyunyiza dawa za asili za kuua kudhibiti wadudu waharibifu mara tu zinapoanza kutoa maua hadi kukomaa. Muulize afisa ugani wako namna ya kutengeneza madawa ya asili yanayokubalika katika mfumo wa kilimo hai.

UKAGUZI WA SHAMBA LA MBEGU
Ili kuhakikisha kuwa taratibu zote zinazotakiwa kufuatwa kwa ajili ya kuzalisha mbegu za kilimo hai zimezingatiwa, shamba la mbegu lazima likaguliwe. Ukaguzi wa nje unafanywa na shirika la Kilimo hai Tanzania na wataalamu kutoka taasisi ya kudhibiti uboa wa mbegu (TPSCI). Wataalamu wa TOSCI wanakagua shamba la mbegu mara tatu kabla y kuchanua, wakati wa kuchanua na kabla ya kuvuna.

UVUNAJI WA MBEGU
Dalili za kukomaa
Wakati wa kukomaa na kukauka vitumba hubadilika rangi na kuwa kahawia.
Namna ya Kuvuna
Vuna kila baada ya siku 3 hadi 5 kwa kuchuma vitumba au kukata matawi.
Kukausha Mbegu
Mavuno yote ambayo yametolewa shambani yapelekwe moja kwa moja kwenye kiwanja cha kukaushia. Ni vizuri sana kukaushia mbegu zilizo vunwa kwenye mkeka au sakafu safi isiyo na unyevunyevu.
Kupura Mbegu
Weka vitumba kwenye gunia halafu upige kwa kutumia fimbo ndogo, ili kuibanguwa.

KUSAFISHA MBEGU
Kutoa uchafu
Peta mbegu kwa kutumia ungo na upepo. Ondoa uchafu wote na mbegu safi ziwekwe kwenye chombo kisafi. Chambua mbegu zilizo kuwa na rangi tofauti na zenye magonjwa zitupwe au zitunzwe kwa ajili ya chakula. Vile vile mbegu zilizonyong'onyea zitengwe.
Kuhifadhi Mbegu
Hifadhi mbegu katika mifuko misafi, mahali penye mzunguko mzuri wa hewa na pasipo wadudu waharibifu. Vichanja huweza kutumika kuzuia mbegu kupata unyevunyevu wa sakafu. Changanya mbegu na majivu ya jikoni au dawa nyingine za asili kudhibiti wadudu. Tunza mbegu mbali na madawa hatari na chakula.