UZALISHAJI WA MBEGU BORA YA KARANGA

Share:

Karanga ni mojawapo ya mazao ya mafuta ambayo hustawi zaidi katika kanda ya kusini, Mashaiki, Kati, na Ziwa. Karanga hutumika kama zao la biashara na chakula.

MAZINGIRA BORA
Hali ya Hewa
- Karanga hustawi vizuri katika nyanda za kati ya 0 - 1500m toka usawa wa bahari na wastani wa mvua mm 500 - 1200 kwa mwaka.
- Karanga huota vizuri kwenye udongo wa kichanga na tifutifu kwa kuwa unaopitisha maji vizuri.

SIFA ZA SHAMBA
Historia ya Shamba
- Shamba ambalo halikulimwa karanga msimu uliopita linafaa kwa uzalishaji mbegu za karanga. Ardhi isiwe ngumu ya kuzuia karanga kubaki ardhini kipindi cha mavuno

Utengaji wa shmba la karanga
Maua ya karanga hujichavusha yenyewe kwa kiasi kikubwa. Hivyo unaweza kutenga mita 3 tu kati ya aina moja na mbegu nyingine bila ya chavua kuingiliana.

Utayaishaji wa shamba
Ukiisha chagua eneo lako tifua na kulainisha ardhi kidogo ili kurahisisha utoaji wa mbegu.

Chanzo cha mbegu
Mbegu zitakazotumika katika uzalishaji zisiwe chotara. Mkulima atumie mbegu ya daraja la msingi, au kuthibitishwa ama QDS 1 . Mbegu ya msingi na iliyothibitishwa hupatikana katika mashamba ya wakala wa mbegu za kilimo ( Agricultural Seed Agency-ASA). Vilevile mbegu za daraja la kuthibitishwa hupatikana katika makampuni ya mbegu, kupitia kwa wakala wao au maduka ya pombejeo.

Mkulima anaruhusiwa ktumia mbegu ya QDS 1 iliyopatikana kutoka kwa mkulima wa mbegu aliye sajiliwa na TOSCI, kama chanzo cha mbegu, lakini ajue ya kwamba, akishavuna hawezi kuitumia kama mbegu tena.

Aina ya mbegu bora zinazopatikana hapa nchini kwa sasa ni Pendo, Johari, Sawia, Mnanje 2009, Mangaka 2009, Maasai 2009 na Nachingwea 2009.

Angalizo
Kwa mkulima anaeanza kuzalisha mbegu, anashauriwa kutumia mbegu ya daraja la msingi.

UPANDAJI
Wakati wa kupanda
- Karanga zipandwe kwa kulenga uvunaji uwe katika kipindi cha mwisho wa mvua ili kurahisisha ukaukaji. Kuchelewa kupanda kunahatarisha mimea kupata ugonjwa na ukoma na madoa ya majani pia wadudu kama kidomozi na inzi wa karanga.

Kiasi Cha Mbegu
Tumia Kilo 32 - 40 kwa ekari, na Kilo 80 - 100 hekta.

Nafasi ya Kupanda
Kupanda kwa nafasi na mstari ndiyo njia muhimu ya kuepusha magonjwa
a) sm 50 x 10 kwa karanga za wima
b) sm 50 x 15 kwa karanga zinazotambaa
c) Shimo liwe na kina cha sm 2.5 - 5

Matumizi ya mbolea
- Rutubisha udongo kwa kutumia mbolea za asili zenye madini ya phosphorus na Calcium kwa ukomaaji mzuri wa karanga.
- Mzunguko wa mazao pia hutunza rutuba ya udongo.

KUSAJILI SHAMBA LA MBEGU
Mara baada ya kupanda, mzalishaji analazimika kusajili shamba lake katika Taasisi ya udhibiti wa ubora wa mbegu (TOSCI) aidha katika kituo cha Migogoro, Njombe au Arusha au sehemu nyingine ambazo taasisi hiyo ina ofisi katika muda usiozidi siku 30 ili kutoa nafasi wakaguzi hao kupanga utaratibu wa ukaguzi.

PALIZI
Muda wote shamba liwe safi. Palizi ya kwanza ifanywe majuma mawili tangu karanga kuota. Palizi ifanyike kwa kutifulia na kulainisha ardhini. Pendelea kung'olea magugu kuepuka kukata mishale ya mizizi. Unaweza kupalilia mara moja au mbili kulingana na wingi wa majani katika eneo lako.

KUNG'OA MIMEA ISIYOFAA NA YENYE UGONJWA
Ondoa mimea isiyofanana na mbegu unayozalisha , pia ng'oa mimea yote dhaifu na iliyopatwa na ugonjwa hasa UKOMA na iliyoharibiwa na wadudu.

Zingatia
Shughuli hii lazima ifanywe kwa kushirikiana na afisa ugani aliye karibu nawe

KUZUIA WADUDU WAHARIBIFU NA WAGONJWA
A) WADUDU
i) Vidukazi (mafuta) Husababisha ugonjwa wa ukoma. Ugonjwa huu hujitokeza zaidi wakati wa kipindi kirefu cha jua au ukame.Mimea iliyoshambuliwa majani yake hukunjamana, hupauka rangi yake na kuwa na njano na hayapanuki. Mimea hudumaa na iking'olewa huwa haina karanga.

Ugonjwa huu hudhibitiwa kwa kupanda mapema na kwa nafasi iliyopendekezwa. Pia mkulima anaweza kupulizia sawa za asili ( utupa, pilipili, mlonge, muarobaini) Kila juma kulingana na mashambulizi.

ii) INZI WA KARANGA
Hufyonza mizizi/mishale ya karanga na karanga changa. Mimea iliyoshambuliwa huwa na rangi ya njano. Ugonjwa huu unadhibitiwa kwa kupanda mapema na kupulizia dawa za asili unapoona mashambulizi katika mashina.

iii) MCHWA
Hutoboa mizizi na kutengeneza matundu wakati mimea ikiwa shambani. Wengine hukata matawi yanayokuwa na kutambaa. Mchwa hawa huonekana zaidi kwenye shamba jipya. Kudhibiti mchwa hawa wasiliana na afisa ugani aliye karibu na wewe akupe maelekezo husika.

B) MAGONJWA
i) Ugonjwa wa kuoza (Aflatoxin)
Unyevu mwingi husababisha vimelea viitwavyo Aspegillus Flavus kuota zikiwa zimekomaa, hali ya unyevu au ukame mkali husababisha ganda la karanga kupasuka na kuruhusu vimelea karanga wakati wa kuvuna. Vile vile karanga zikaushwe vizuri na kuhifadhiwa kwenye magunia na siyo viroba katika sehemu isiyokuwa na unyevunyevu.

ii) Ugonjwa wa madoa ya majani na kutu
Husababishwa na vimelea vya uyoga. Ugonjwa huu hujitokeza zaidi katika wiki ya 3-5 baada ya karanga kuota na ugonjwa wa kutu ya majani hujitokeza wiki ya 5 na karibu ya kukomaa. Ugonjwa huu unadhibitiwa kwa kupanda mapema, kuondoa maotea, kilimo cha mzunguko na kutumia mbegu bora zinazostahimili magonjwa.

iii) Ugonjwa wa Ukoma (Resette Virus Disease)
Huambukizwa na wadudu mafuta (Aphids). Ugonjwa huu husababisha mimea kudumaa, majani kukunjamana kama ukoma na huwa na rangi ya njano au kijani. Ugonjwa huu hudhibitiwa kwa kupanda mapema na kwa nafasi, kupalilia kwa wakati, kutoa maotea na kutumia mbegu bora

iv) Ugonjwa wa Maganda Matupu (empty pods)
Ugonjwa huu husababishwa na ukosefu wa madini ya chokaa (kalsiam) katika udongo. Karanga hushindwa kujaa kwenye udongo na kutumia mbegu za muda mfupi.

Uvunaji wa mbegu
. Mazao yavunwe mara baada ya ukaguzi wa mwisho
. Vuna karanga zilizokomaa. Dalili za mbegu ya karanga iliyokomaa ni maganda yake ndani hubadilika kutoka weupe kuwa na rangi ya khaki. Majani ya chini huwa rangi ya njano na kuanza kupukutika.

Namna ya Kuvuna
Ng'oa karanga kwa mikono kwenye ardhi tifutifu na jembe katika eneo lenye udongo mzito.

Ukaushaji
Kausha mbegu kwa kugeuza shina chini kuwa juu ili zisiweze kukauka. Pia unaweza kuanika kwenye kichanja.

Kuhifadhi mbegu
. Karanga zitunzwe na maganda yake hadi msimu wa kupanda unapokaribia.
. Chumnba cha kutunzia mbegu kisiwe na matundu yanayoweza kuruhusu wanyama waharibifu kama panya kupita lakini kiwe kinapitisha hewa kwa urahisi. Pata ushauri wa wataalam wa kilimo nhaikatika matumizi ya mbinu/madawa ya asili kwa ajili ya kuhifadhi mbegu.

Vifaa vya Kuhifadhia Mbegu
. Karanga zitunzwe na maganda yake hadi msimu wa kupanda unapokaribia.
. Chumba cha kutunzia mbegu kisiwe na matundu yanayoweza kuruhusu wanyama waharibifu kama panya kupita lakini kiwe kinapitisha hewa kwa urahisi. Pata ushauri wa watalam wa kilimo hai katika matumizi ya mbinu/ madawa ya asili kwa ajili ya kuhifadhi mbegu.

Vifaa vya kuhifadhia mbegu
.Tumia vifaa safi, kama vile magunia yanayopitisha hewa (jute)
.Panga maguniua yasigusane na ukuta na sakafu ili kuruhusu mzunguko wa hewa na ukaguzi.

KUPIMA UBORA WA MBEGU
Mara baada ya kuvuna, kusafisha na kuhifadhi vizuri na kabla ya mbegu kuruhusiwa kuuzwa ni lazima ipimwe ubora wake kwa mfano, utoaji, usafi wa mbegu n.k Kazi ya kupima ubora wa mbegu inafanyika kwenye maabara ya mbegu katika Taasisi ya udhibiti ubora wa mbegu (TOSCI). Afisa wa TOSCI au wakala wake atachukua sampili ya mbegu na kuzipeleka maabara ya mbegu ya TOSCI kwa ajili ya kuthibisha ubora wake. Mbegu ikithibitika kama ina ubora unaotakiwa inaweza kuuzwa. Baada ya matokeo ya maabara mkulima anatakiwa kujaza fomu ya kuazimia ubora wa mbegu.

Zingatia
Iwapo mbegu itabaki baada ya msimu kuisha itabidi sampuli nyingine ya hiyo mbegu ichukuliwe na ipelekwe  TOSCI kabla ya kuiuza kwa msimu ujao. Hii ni kuhakikisha kuwa mbegu hiyo bado ina uwezo wa kuota.

UUZAJI WA MBEGU
Iwapo majibu kutoka taasisi ya udhabiti wa ubora wa mbegu yakarudi mazuri basi mbegu hi inaweza ikauzwa. Fungasha mbegu yako katika vipimo vya kilo 1,2,5 na kadhalika kufuatana na mahitaji ya soko. Mzalishaji anashauriwa kutumia mifuko ya nailoni, karatasi ngumu au viroba. Mbegu itakayobaki baada ya msimu kwiusha itabidi ichukuliwe sampuli tena kabla ya msimu mwingine kuanzaili kufanyiwa majaribio ya utoaji, ijulikane kama inafaa kuuza kama mbegu.