FAIDA YA TUNDA LA MKOMAMANGA KWA AFYA YA BINADAMU
Mkomamanga (Punica granatum)ni mmea ambao asili yake ni katika nchi za Mashariki ya Kati (Middle East)
Mkomamanga una dawa mbalimbali kama vile Tannis (punicalin na punicalagin), Flavonoids, Alkaloids, Steroids, Triterpenes na Polyphenols. Dawa hizi hupatikana katika magome, majani, mbegu, maganda ya matunda, juisi ya matunda na katika maua ya mkomamanga. Tunda la komamanga pia lina vitamini C na E kwa wingi pamoaja na madini ya potassium na copper.
mkomamanga pia ni mti unaozaa matunda ambayo maganda yake huchemshwa na kufanywa dawa ya kufunga kuhara (TUKI, 1981).
Faida ya tunda hili ni kama zifuatazo;
Lojo ya mbegu za matunda ya komamanga ikichanganywa na maziwa, husaidia katika tiba ya kuondosha mawe katika figo. Fukuto ya Mkomamaga husaidia katika tiba ya minyoo aina ya tegu (Tapeworms) lakini pia husaidia katika matibabu ya uvimbe wa wengu (Spleen). Dawa-lishe hii pia husaidia kwa kiwango kikubwa katika uponaji wa vidonda vya tumbo.
Komamanga pia ni mahili katika tiba na kuzuia magonjwa ya kusendeka (magonjwa ya muda mrefu) kama vile saratani ya tezi ya prosteti ya wanaume, saratani mbalimbali, kisukari, baridi yabisi na uvimbe wa maungio ya vidole (gout). Komamanga husaidia mwili kuondosha sumu na uchafu utokanao na kemikali na mabaki ya vyakula mwilini kama vile asidi ya uriki (uric acid). Sumu hizi ni chanzo kikuu cha magonjwa mengi ya kusendeka.
Dawa zinazopatikana katika maganda na majani ya mkomamanga husaidia katika matibabu ya hali ya tumbo kujaa gesi na kudhibiti tindikali (acid) tumboni. Mkomamanga pia husaidia katika matibabu ya kuhara damu na kutibu uambukizo katika kibofu cha mkojo (Cycititis).
Katika mfumo wa damu, komamanda hutoa msaada mkubwa wa kuzuia na kutibu magonjwa yanayoshambulia mfumo huo nyeti. Komamanga ni dawa nzuri ya kuzuia na kutibu shinikizo la damu, magonjwa ya nyama za moyo, kiharusi (Cerebrovascular Accident) na magonjwa ya mishipa ya damu. Komamanga lina madini aina ya potassium na copper kwa wingi, pamoja na faida zingine mwilini, madini haya husaidia kusharabiwa (kufyonzwa)kwa madini ya chuma kutoka katika utumbo kwenda mwilini kwa urahisi na hii husaidia katika matibabu na kinga ya tatizo la upungufu wa damu mwilini.
Katika majaribio ya kisayansi imethibitika kuwa juisi ya komamanga na fukuto ya mmea huu husaidia kudhibiti kasi ya kuzaliana kwa virusi vya UKIMWI namba 1 [HIV-1]. Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Neurath A. R pamoja na wenzake na kupewa kichwa kisemacho “Punica granatum juice provides an HIV-1 inhibitor and candidate tropical microbicide”. Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la kisayansi la BMC infectious diseases (4) 41-45(2004). Matokeo yanayofanana na hayo pia yalithibitika katika utafiti mwingine uliofanywa na Kun Silprasit na wenzake mnamo mwaka wa 2011 na kupewa jina la “Anti-HIV-1 Reverse transcriptase activities of hexane extracts from Asian Medicinal Plants”. Utafiti huo ulichapishwa katika jarida la kisayansi la “Journal of Medical Plant Research Vol. 5 (17), pp. 4194-4201, 9 Sept 2011”.