MADHARA YA WADUDU WAHARIBIFU WA NYANYA

Share:

Kufahamu kuhusu wadudu waharibifu katika mimiea ya nyanya kama mkulima unatakiwa uwe unachunguza mimea yako mara kwa mara. Angalia uwepo wa wadudu kwenye sehemu ya chini ya majani, juu yake, kwenye mashina, maua au matunda kama yametobolewa au la.

Aina ya wadudu waharibifu wa nyanya ni kama wafuatao


Minyoo Fundo: Root knot nematodes (Meloidogynespp.)

Dalili za minyoo fundo husababisha umanjano na kudumaa kwa mimea na hatimaye kunyauka wakati wa jua kali. 
Mashambulizi ya hawa wadudu husababisha kupungua kwa mazao ikitegemea ukubwa wa mashambulizi kwenye mizizi, mashambulizi makubwa husababisha kufa kwa mimea. 

Dalili za ugonjwa ni mizizi huonekana umevimba na yenye maumbile mabaya na vifundo, yanayojulikana kama mafundo ya mizizi. Mashambulizi makubwa husababisha mzizi wote ukawa na umbile baya na mafundo ambao hatimaye huoza. Mashambulizi yanayofuata husababisha uharibifu na dalili za magonjwa huongezeka kwenye nyanya.

Mbinu bora za kudhibiti wadudu/ugonjwa
- Tumia mimea ya mitego kama vile Mbange ‘marigold’ (Tagetes spp.) na haradali ya India.

- Dumisha kiwango kikubwa cha mbolea za asili (samadi na mboji) katika udongo.

- Changanya mashudu (mabaki) ya muarobaini na udongo.

- Tumia aina zenye kustahimili minyoo fundo (kama Caracas, Kentom, Meru, Piersol, Roma VFN, Tengeru 97, Zest F1, Star 9001 na Star 9003).

- Zungusha mazao na vitunguu maji, mahindi madogo, mahindi matamu, mahindi, mtama, uwele, ufuta, au nyasi. Mbinu ya mzunguko wa mazao unaojulikana kama “STRong” unashauriwa kutumika katika udhibiti wa minyoo fundo. Mbinu hii inashauri kupandwa kwa mmea usiostahimili (kama Nyanya), ikifuatiwa na zao lenye kustahimili kidogo (kama Kebeji), halafu zao lenye kustahimili kabisa (kama Vitunguu maji), kabla ya kurejea tena zao lisilostahimili (kama Nyanya).

- Ng’oa mizizi na uchome moto mimea iliyoathirika na takataka zote za mazao.

- Ua vimelea vya maradhi kwenye vitalu kwa kutumia moto au mvuke kabla ya kusia mbegu.

- Epuka kupandikiza miche iliyoathirika.

- Tumia mbinu za kibaiolojia kwa kutumia bidhaa zinazotokana na Trichoderma.

Funza wa vitumba: American bollworm (Helicoverpa armigera)
Funza wa vitumba  kwanza hula majani baadae huingia ndani ya matunda na kusababisha uharibifu mkubwa. matunda machanga husababisha kupukutika kwake, wakati mashambulizi ya matunda yaliyokomaa husababisha matundu ambayo huruhusu kuingia kwa aina nyingine za ukungu na bakteria ambao huleta madhara zaidi.

Mbinu bora za kudhibiti wadudu/magonjwa
- Chuma na teketeza matunda yaliyoathirika.
- Ondoa na teketeza mabaki ya mazao baada ya kuvuna.
- Chimbulia ardhi baada ya mavuno.
- Fanya mzunguko wa mazao.
- Toa kwa mkono na teketeza mayai na funza wadogo wadogo.
•Epuka kupanda nyanya karibu na pamba au mahindi.
•Changanya mazao, panda na pilipili na maua bange (African marigold).

Vidukari au Wadudu mafuta (Aphids)

Ni wadudu wenye rangi nyeusi au kuijani au kahawia. Hukaa chini ya majani na kufyonza utomvu kwenye majani machanga. Hudumaza mmea na kushindwa kuzaa matunda. 

Mbinu bora za kudhibiti wadudu/magonjwa
Nyunyizia maji ya majani ya mwarobaini na utupa, maji ya pilipili.

Utitiri Mwekundu: Red spider mites  (Tetranychus urticae)
Utitiri huu unaweza kutambulika kwa kutumia lenzi ya mkono na pia huwa ni tatizo hasa wakati wa kiangazi. . Dalili za awali hujumuisha madoa ya manjano, ambayo hujitokeza pale mashambulizi yanapokuwa makubwa; baada ya hapo huja ishara ya kuungua kwenye majani na matunda ikifuatiwa na utando kama wa buibui.

Mashambulizi mengine ni kiwango kikubwa cha  umanjano wa majani na matunda, kupukutika mapema kwa majani, kukauka kwa mti kuanzia kileleni na kufa kwa mmea. 

Vichungu vya utitiri wekundu hujikusanya kwenye ncha za majani wakati idadi ya utitiri wekundu inapozidi chakula kilichopo.

Sota (Cutworms)
Hushambulia miche ya nyanya hasa baada ya kupandikizwa shambani. Wakati wa mchana hujificha kwenye udongo na usiku hujitokeza na kukata miche kwenye shina usawa wa udongo.

Namna ya kudhibiti
Hakikisha miche inapata maji ya kutosha

- Nyunyiza dawa zisizo na kemikali za kuua wadudu kwenye shina usawa wa udongo