Fahamu madhara yanayosababishwa na Panya kwenye Mazao Shambani

Share:
Panya ni wanyama wadogo jamii ya mammalia walio katika familia/kundi linalotambulika kitaalamu kama Muridae wenye meno mawili ya mbele kwa kila taya na mwanya kati ya meno ya mbele na magego unaotambulika kitaalamu kama Diastema.

Aina Za Panya
Panya wa Darini (Rattus rattus)

Hii ni aina ya panya waharibifu wanaoishi majumbani ambao hupendelea sana kukaa katika paa la nyumba 
Panya Shamba (Mastomys natalensis)
Panya shamba ni aina ya panya waharibifu wanaosababisha hasara kubwa kwa wakulima panya hawa huishi mashambani na porini na hupatikana sana sana katika jangwa la sahara. Majike wa aina hii ya panya wanaweza kuzaa watoto ishirini kwa mkupuo. Panya wa aina hii hushambulia mazao ya nafaka, mazao ya mizizi, mazao jamii ya kunde pamoja na zao la pamba. Panya hawa wanapendelea kula mbegu zilizofukiwa shambani, miche, mazao yaliyokomaa.
Madhara Yanayosababishwa Na Panya
Panya wasipodhibitiwa huweza kumsababishia mkulima hasara kubwa kwa kula mbegu za mazao zilizopandwa kwa kufukua mashimo na  mazao yaliyo kuwa shambani. Vilevile panya wana uwezo wa kula mazao yaliyoifadhiwa katika maghala.
Panya hupendelea sana kula;
- Mazao ya mafuta kama vile alizeti na karanga
Mbegu za mazao ya mboga kama vile matikiti, maboga
Mazao ya nafaka kama vile mahindi, mpunga na mtama
Mazao ya mboga kama vile nyanya na matango
Mazao jamii ya kunde kama vile mbaazi, maharage na kunde
Pia panya wana uwezo kusababisha magonjwa mbalimbali kwa binadamu Tauni, typhoid, paratyphoid magonjwa hayo huenezwa kwa kupitia vinyesi na mikojo ya panya, panya kunusa au kulamba vyombo vya jikoni au kupitia utitiri na viroboto wa panya wanaoweza kuwauma wanyama na binadamu.
Ukaguzi Wa Shamba
Kabla ya kuelezea ni mbinu gani utumie katika kukabiliana na mlipuko au uvamizi wa panya katika shamba lako ningependa ujue kuwa kufanya ukaguzi wa shamba ni sehemu muhimu sana katika udhibiti wa panya kwani kwa kufanya ukaguzi unaweza kutambua uwepo wa panya katika shamba lako, maficho yao na chanzo cha tatizo ili kuweza kuchukua hatua stahiki.
Ukizingatia tabia ya panya kupenda kuishi kwa makundi katika sehemu tofauti za eneo moja fanya ukaguzi katika sehemu zote za shamba lako kati, pembezo na maeneo mengine yote ya karibu na shamba na endapo utabaini maficho ya panya sehemu fulani hakikisha unaendelea na ukaguzi hadi utakapokamilika kwani kuna uwezekano mkubwa wa uwepo wa maficho ya panya sehemu nyingine. Kama ilivyoelezwa katika sehemu ya tabia za panya kwa kawaida mashambulizi ya panya ni matokeo ya panya walio katika maficho mawili au zaidi katika eneo moja hivyo maeneo yote ndani ya shamba na karibu na shamba yana umuhimu sawa katika zoezi la ukaguzi. Kwa mantiki hiyo zoezi hili ni busara likahusisha jamii nzima kwa eneo husika ili kuongeza ufanisi.
Inashauriwa ukaguzi wa shamba ufanyike mara kwa mara ili kuweza kubaini mapema uwepo wa panya kabla idadi yao haijawa kubwa ambapo kwa upande wa muda unaofaa kufanya ukaguzi ili kuwaona panya kwa urahisi katika shamba lako ni wakati wa asubuhi, jioni au usiku kwa kutumia tochi kama ukiweza. Muda huu ndio ambao panya hupendelea kutembea na kula mazao katika mashamba. Wakati wa kufanya ukaguzi katika shamba lako ni vyema kuzingatia viashiria vya uwepo wa panya vinavyoweza kuonekana.
Vishiria vya Uwepo wa Panya katika shamba
Uwepo wa panya katika shamba au mahali popote huwa na viashiria vinavyoonekana kutokana na shughuli za panya katika eneo husika. Ni muhimu sana kuvijua viashiria hivi kwani vinaweza kukusaidia wakati unapofanya ukaguzi wa shamba. Wakati mwingine kiashiria kimoja kinaweza kisikupe majibu sahihi juu ya uwezekano wa kuwepo uvamizi wa panya katika shamba lako hivyo ni busara kuzingatia viashiria zaidi ya kimoja kabla ya kusema shamba limevamiwa au la. Unapoona kuna viashiria vifuatavyo katika shamba lako jua ya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa uwepo wa panya.
Mazao yaliyoshambuliwa na panya
Mazao yaliyoshambuliwa na panya katika shamba lako ni ishara tosha ya uwezekano wa kuwepo kwa panya shambani kwa mfano, katika bustani ya nyanya unaweza kukuta mabaki ya nyanya zilizoliwa au kukuta mahindi yamegugunwa kutoka katika magunzi yakiwa shambani.  Vilevile mabaki ya mbegu zilizoliwa kiini kwa mazao mbalimbali ya nafaka kama vile mahindi na mashina ya mimea yaliyoliwa kama vile mashina ya miwa ni ishara kuwa mazao hayo yameshambuliwa na panya.
Njia za panya
Panya kwa kawaida wanapovamia eneo fulani hutengeneza njia zao ambazo huzitumia mara kwa mara wakati wanapotafuta mahitaji yao mbalimbali. Njia hizi mara nyingi huelekea hadi yalipo maficho yao na hivyo wakati wakufanya ukaguzi unaweza kufuata njia hizi na kuweza kubaini maficho ya panya wanaoshambulia mazao katika shamba lako.
Mashimo yaliyopandwa mbegu kufukuliwa
Panya kama nilivyokuelezea hapo awali wana uwezo wa kufukua mashimo yaliyopandwa mbegu za mazao mbalimbali na kula mbegu hizo hata kabla ya kuota. Hivyo unapokuta mashimo yamefukuliwa na mbegu kuliwa kabla ya kuota jua ya kuwa shamba lako limevamiwa na panya.
Panya wazima au mizoga

Panya wazima wanaweza kuonekana kwa urahisi ikiwa utafanya ukaguzi wakati ambao wao hupendelea kutembea kama ilivyoelezwa hapo juu. Kwa makadilio ukimwona panya mmoja awe mzima au amekufa katika shamba ujue kuna uwezekano wa kuwepo panya wengine 25 au zaidi ambao bado haujawaona.
Vinyesi na madoa ya mikojo ya panya
Kwa kawaida vinyesi vya panya vina ukubwa tofauti kutegemeana na aina ya panya lakini ukubwa wake unalingana kwa karibu na ukubwa wa punje moja ya mchele hadi mbegu moja ya maharage. Vinyesi vya panya kwa aina za panya karibu zote vinapokuwa vibichi huonekana vyenye unyevu na rangi ya kung’aa lakini vinapokauka hubadilika rangi na kuwa na rangi nyeusi.
Michirizi ya mikojo na vinyesi vya panya vinaweza kuonekana katika sehemu tofauti ndani ya mipaka ya makundi ya panya hasa katika njia zao na kwa maeneo utakayokuta idadi kubwa ya vinyesi vya panya ujue maeneo hayo ndiyo wanayopendelea zaidi kuyatembelea. Vilevile kwa kufuatilia michirizi ya mikojo na vinyesi vya panya unaweza kugundua kwa urahisi njia za panya na maficho yao
Mashimo au maficho ya panya
Kama ilivyoelezwa katika sehemu ya tabia za panya kwamba panya hupendelea kuishi katika maeneo yaliyojificha ili kujikinga na maadui (predators) na kuweza kuzaliana kwa usalama kuwepo kwa mashimo au maficho ya panya sehemu yoyote ndani au maeneo ya karibu na shamba ni ishara wazi kwamba katika eneo hilo kuna uvamizi wa panya.
Milio ya panya
Panya wana uwezo wa kutoa sauti kali ya milio inayoweza kusikika hadi kufikia umbali mrefu kidogo. Kwa sababu hiyo unaposikia milio ya panya katika sehemu tofauti katika shamba lako au maeneo mengine elewa kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa panya mahali hapo.