Magonjwa ya pilipili hoho ni moja ya sababu kuu zinazoweza kusababisha hasara kubwa sana katika kilimo cha pilipili hoho. Hasara ya mpaka asilimia mia inaweza kutokea kama hatua za kuyadhibiti magonjwa ya pilipili hoho hazitachukuliwa mapema.
Hivyo ili mkulima aweze kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na magonjwa ni muhimu ajue ni magonjwa yepi yanasumbua sana zao hili la pilipili hoho. Yafuatayo ni magonjwa ya pilipili hoho na njia za jinsi ya kuyadhibiti;
i. Chule (Anthracnose)
Huu ni ugonjwa wa ukungu unaoanzia kwenye mbegu husababishwao na fangasi (Colletotrichum spp). Ugonjwa huu huweza kushambulia zao la pilipili hoho katika hatua zote za ukuaji hata baada ya kuvuna na mara nyingi hutokea wakati bustani inapokua katika hali ya unyevu mwingi.
Dalili
Ugonjwa huu husababisha madoa yaliyo bonyea yenye maji ambayo baadae hutanuka na kuwa meusi yenye viduara vya kahawia.
Udhibiti
Hakikisha unatumia mbegu safi zisizo na maambukizi ya ugonjwa. Epuka msongamano kwa kupandikiza kwa nafasi miche isiyo na ugonjwa shambani na pia usimwagie maji majani ya mimea kuepuka kuongeza hali ya unyevu bustanini.
ii. Ubwili unga (Powderly mildew)
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya fangasi (Laveillula taurica) vinavyo shambulia mazao ya aina nyingi. Ugonjwa huu hupendelea hali ya hewa ya joto ambapo huweza kuonekana hata pale ambapo shamba linapokuwa katika hali ya ukavu.
Dalili
Utaona unga unga wa rangi ya kijivu chini na juu ya majani ya mmea ya majani yaliyokomaa na baadaye hushambulia majani machanga. Baada ya muda majani hubadilika rangi taratibu kuwa ya njano na mwishowe hufa na kupukutika.
Udhibiti
Njia nzuri ya kudhibiti ugonjwa huu ni kuenea kwa dawa za asili zinazotokana na mafuta ya kitunguu saumu au muarobaini huweza kutumika.
iii. Batobato
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na virusi unaoenezwa kwa urahisi na wadudu wanaokula kwa kufyonza utomvu wa mmea kama vile vidukari na nzi weupe.
Dalili
Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kudumaa na kukunjamana kwa majani. Vilevile majani hubadilika rangi taratibu kutoka kijani, kijani kilichofifia mpaka rangi ya njano katika michirizi.
Udhibiti
Ugonjwa huu huweza kudhibitiwa kwa kupanda aina ya pilipili hoho zinazostahimili ugonjwa kama vile Yolo wonder na kung’oa miche inayoonyesha dalili za ugonjwa. Vilevile. Hakikisha bustani yako ipo mbali na shamba la tumbaku au matango. Teketeza masalia yote ya mazao baada ya kuvuna.
iv. Bakadoa (Bacterial Leaf spot)
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya magonjwa aina ya bakteria (Xanthomonas campestris pv. Vesicatoria) na kuenea kwa njia ya mbegu, mvua na umande. Ugonjwa huu hushambulia majani, shina na matunda.
Dalili
Majani huanza kuwa na madoa madogo ya rangi ya njano yasiyo na umbo maalum yenye maji maji na kingo nyeupe nyembamba ambayo hubadilika taratibu na kuwa ya kahawia katikati na mwisho wa ugonjwa huu majani hupukutika. wakati mwingine madoa yanapokuwa mengi majani huweza kupukutika wakati yakiwa bado na ukijani. Madoa ya kwenye matunda huonekana madogo ya duara na yaliyodidimia yenye rangi ya kahawia hadi nyeusi.
Udhibiti
Unaweza kuzuia ugonjwa huu kwa kupanda mbegu zilizothibitishwa na wataalam na kunyunyizia dawa zenye viambato vya Mancozeb au copper.Hakikisha bustani inakuwa katika hali ya usafi wakati wote na teketeza masalia yote ya mazao baada ya kuvuna. Usimwagie maji juu ya mmea wakati wa kumwagilia.
Kuoza kitako (Blossom end rot).
Hii ni hitilafu inayotokana na upungufu wa virutubisho vya chokaa (calcium) kwenye mmea ambapo huathiri matunda ya mmea. Kuoza kitako kunasababishwa na kiwango kidogo cha maji katika udongo na utaratibu mbaya wa umwagiliaji.
Dalili
Dalili za tatizo hili huonekana zaidi kwenye matunda ambapo sehemu ya chini ya tunda hubadilika rangi na kuwa ya kahawia kabla ya kuoza.
Udhibiti
Mwagilia bustani kiwango cha kutosha cha maji na hakikisha unakuwa na ratiba moja maalum ya umwagiliaji bila ya kubadili badili. Usiache udongo ukakauka kabisa kabla ya kumwagilia. Punguza matumizi ya mbolea za Naitrojeni bustanini hasa baada ya maua kutoka. Tumia CAN kama mbolea ya kukuzia miche bustanini na punguza majani katika mche wenye majani mengi kwa kupogolea (pruning).
Hitilafu zingine zinazoweza kuathiri zao la pilipili hoho ni pamoja na kuungua kwa matunda kunakotokana na mionzi ya jua na kupasuka kwa matunda.