Mbolea ya Mboji na Faida Zake

Share:
Mboji ni aina ya mbolea ya asili yenye rangi nyeusi na harufu nzuri ya kidongo ambayo hutokana na kuoza kwa mchanganyiko wa masalia ya mimea kunakosababishwa na vijidudu na wadudu rafiki wa mazao.
JINSI YA KUCHEKECHA MBOLEA YA MBOJI
Mbolea ya mboji iliyoiva ichekechwe katika chekecho lililotengenezwa kwa wavu kama vile unachekecha mchanga au udongo ili kuisafisha kwa kuondoa vipande vya miti ambavyo havijaoza.
MATUMIZI YA MBOLEA YA MBOJI SHAMBANI
  • Mbolea ya mboji kama Kiboresha udongo
Mboji inapotumika kama kiboresha udongo huchanganywa na udongo katika shamba ili kuboresha tabia za udongo muhimu kwa ustawi wa mazao. Mbolea ya mboji iliyoiva vizuri isambazwe shamba zima kwa kiwango kitakachotegemeana na kiasi kilichopo kisha ilimiwe pamoja na udongo. Mboji ikitumika kama kiboresha udongo ni muhimu isambazwe katika shamba zima kwa sababu lengo ni kuboresha tabia ya udongo wa shamba zima na sio sehemu fulani ya shamba hivyo kwa kiwango unachoweza kumudu hichohicho sambaza katika shamba zima.
Mbolea ya mboji inapotumika kama kiboresha udongo huweza pia kufanya kazi kama mbolea kwa kutoa virutubisho vinavyohitajika kwa ustawi wa mazao lakini inashauriwa usiache kuweka mbolea nyingine kama samadi au mbolea za viwandani ili kutosheleza mahitaji ya virutubisho.

  • Mbolea ya mboji kama Matandazo
Mboji ambayo haijaiva vizuri hutumika kama matandazo kwa kuwekwa na kutandazwa juu ya udongo katika shamba kabla au hata baada ya kupanda. Mbolea ya mboji iliyowekwa kama matandazo huendelea kuoza taratibu huku ikirutubisha udongo na mazao shambani. Ukiweka mboji kama matandazo katika kitalu cha mboga husaidia miche kukua vizuri kwa kuwa sio tu kwamba itarutubisha miche bali itaongeza pia uwepo wa hewa ya Carbon dioxide inayozalishwa wakati wa kuoza kwa malighafi ambayo ni muhimu kwa utengenezaji wa chakula cha mmea.
Matumizi ya mbolea ya mboji kama matandazo huharakisha matumizi ya mboji badala ya kusubiri kwa muda mrefu hadi iweze kuiva kabisa. Mbolea ya mboji inaweza kutumika ikiwa katika awamu ya kupoza au kabla ya kukamilika kwa awamu ya kupevuka. 
  • Mboji kama Mbolea
Mboji huweza kutumika kama mbolea kwa sababu ina virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mmea katika viwango tofauti hasa virutubisho vya msingi vya Naitrojen, Fosfati na Potashi (N.P.K). Mboji kama mbolea huweza kutumika hata kabla ya kuiva vizuri kwa kuwekwa juu ya udongo kuzunguka shina la mmea au ikiwa imeiva kwa kuichanganya na udongo katika shamba zima au katika mashimo ya kupandia. Mara nyingi ni vigumu kutengeneza mboji yenye wingi wa kutosha kusambazwa shamba zima hasa lenye ukubwa wa ekari moja au zaidi hivyo ni busara kuweka mboji kama mbolea katika mashimo ya kupandia.

Matumizi ya mbolea ya mboji katika kilimo cha mazao yana faida zifuatazo;

      - Mboji huongeza uwezo wa udongo kutunza maji na hivyo kupunguza kasi ya ukaukaji wa udongo hasa katika maeneo yenye hali ya joto na yasiyopata mvua za kutosha.

        - Mbolea ya mboji huboresha afya ya mmea na kufanya uwe na uwezo wa kustahimili magonjwa

       - Mbolea ya mboji huongeza virutubisho vinavyohitajika na mmea katika udongo na hivyo kuongeza mazao.


  1. Mbolea ya mboji huweza kutumika kama mbadala wa mbolea ya samadi wakati wa kuandaa kitalu cha mboga.


  1. - Mbolea ya mboji huboresha muundo wa udongo unaopelekea kuwa na mzunguko mzuri wa hewa na maji katika udongo.