KUCHAGUA MAYAI YA KUANGUA.
Hili nalo ni muhimu kuzingatia. Ni vizuri kuchagua mayai ya kuatamia ili mayai yasiyofaa yaweze kuuzwa au kutumiwa nyumbani kwa chakula. Mayai ya kuatamia yawe na sifa zifuatazo
Yasiwe na uchafu yawe masafi
Yasiwe na nyufa
Yatokane na kuku aliyepandwa na jogoo
Yasiwe madogo wala makubwa bali yawe na ukubwa wa wastani kulingana na umbile la kuku.
Yasiwe mviringo kama mpira pia yasiwe na ncha kali sana.
Yasiwe yamekaa muda mrefu zaidi ya wiki mbili toka yalipotagwa
Yasiwe yaliyohifadhiwa kwenye sehemu yenye joto.
KUMTAYARISHA KUKU WA KUATAMIA
Pamoja na matayarisho hayo zingatia kumuwekea mayai yasiyozidi 15 pia ni vizuri yasipungue 12. Kuku wanaotazamiwa kuatamia ni lazima wachunguzwe kwa makini kabla ya kuatamia ili kuhakikisha kwamba hawana chawa, utitiri n.k. Kuwepo kwa wadudu hao huwafanya kuku wakose raha na kutotulia kwenye viota vyao. Hali hii husababisha kuanguliwa kwa Vifaranga wachache.
Sasa unatakiwa kufanya yafuatayo:-
Nyunyiza dawa ya kuua wadudu ndani ya kiota
Pia mnyunyuzie dawa kuku anayetarajia kuatamia
Weka mayai kwenye kiota huku mikono yako ikiwa imepakwa jivu ili kuepuka kuwa na harufu kwani kuku anaweza kuyasusa.
Ni vizuri kuifanya kazi hii ya kumuandaa kuku anayetaka kuatamia wakati wa usiku. Pia ifahamike kuwa kwa kawaida kuku huatamia mayai yake siku 21.
PIA JIFUNZE MBINU ZA KUATAMIA MAYAI MENGI KWA NJIA ZA ASILI.
Iwapo una kuku wengi wanaotaga kwa wakati mmoja ni vema ukawafanya wakaatamia na kutotoa pamoja.
Unachotakiwa kufanya ni kuchagua mayai ya kuatamia ukianzia na yai la mwisho kutaga.
Unaweza kuwaandaa kuku wako zaidi ya mmoja ili waanze kuatamia kwa pamoja na kupata vifaranga vingi kwa mara moja kuku wa kwanza anapoanza kuatamia. Mwekee mayai viza au ya kuku wa kisasa kwani kuku huatamia hadi mayai yanapoanguliwa hivyo ukimuwekea mayai yasiyo na mbegu atakaa hapo muda mrefu hadi vifaranga watoke.
UTEKELEZAJI WAKE.
Kuku anapotaga kila siku weka alama ya namba au tarehe kulinganisha na siku anayotaga
Yanapofika mayai matatu yaondoe na muwekee mayai viza au ya kisasa huku ukiendelea kuweka alama mayai yanayotagwa kila siku.
Mara kuku anapoanza kuatamia muongezee mayai ya uongo yafikie 8 hadi 10
Fanya hivyo kwa kila kuku anayetaga hadi utakapoweza kupata idadi itakayoweza kukupatia vifaranga wengi kwa wakati mmoja.
Wawekee kuku wote mayai siku moja kwa kuondoa mayai ya uongo na kuwawekea mayai ya ukweli wakati wa usiku.
MUHIMU.
Mayai ya kuatamia yasishikwe kwa mkono ulio wazi na wala yasipate harufu za mafuta ya taa, manukato n.k.
JIFUNZE PIA KUTAMBUA MAYAI YALIYO NA MBEGU NA YALE YASUYO NA MBEGU.
Mfugaji anaweza kutambua mayai yaliyo na mbegu na yale yasiyo na mbegu siku ya saba baada ya kuanza kuatamia iwapo atapima mayai kwa kutumia box lililotengenezwa maalum pamoja na tochi yenye mwanga mkali ndani ya chumba chenye kiza. Hii itamuwezesha mfugaji ayatumie mayai yasiyo na mbegu kwa chakula cha familia au kuyauza.