Namna Kudhibiti magonjwa ya mazao kwa njia za asili

Share:
Kuna madhara mengi yatokanayo na matumizi ya dawa za viwandani zenye sumu. Madhara hayo ni pamoja na athari za afya kwa binadamu, wanyama, mimea, na uharibifu wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji.

Dawa za asili zinazoweza kusaidia kudhibiti magonjwa ya mazao 
Vitunguu saumu
 Dawa hii hutumika kufukuza wadudu kutokana na harufu yake. Chukua gramu 100 za vitunguu, twanga vilainike, changanya na maji lita mbili. Chuja kisha nyunyiza kwenye mimea. Dawa hii pia inaweza kuchanganywa na mojawapo ya dawa za asili, ili kutoa harufu kali itakayofukuza wadudu.

Majivu 
Weka majivu moja kwa moja kwenye mashina ya mimea michanga baada ya kuotesha ili kuzuia wadudu wakatao mimea michanga. Majivu huonyesha matokeo mazuri endapo yatachanganywa na mafuta ya taa kidogo.

Ndulele/ ndula 
Chukua matunda ya ndulele 30 au 40 haijalishi yameiva au mabichi. Katakata na uyakamue ili kupata juisi. Ongeza lita moja ya maji, koroga sawa sawa kisha chuja. Ongeza maji lita mbili. Tumia lita moja ya dawa kwa lita 15 za Maji kisha nyunyiza mimea mara mbili kwa wiki.

Pilipili kali
 Hii ni moja ya dawa za asili ambazo zimekuwa zikitumika na kwa ufanisi mkubwa. Dawa hii inapotengenezwa na kutumika kwa umakini huwa na ufanisi mkubwa zaidi katika udhibiti wa wadudu na magonjwa. Chukua gramu 55 za pilipili. katakata vipande vidogo vidogo kisha chemsha kwa dakika 20 kwenye maji ya lita tano. Chuja kisha ongeza maji lita 5 Dawa hii huua wadudu wenye ngozi ngumu (mbawa kavu) na laini kama vidukari, wadudu wa kabichi na wengineo.

Tumbaku 
Tumia ugoro au chemsha miche 20 ya tumbaku. Dawa hii inazuia wadudu wanaoshambulia mahindi shambani, wadudu wanaokata miche, kupe, vidukari, viwavi na wengineo. Chukua gramu 500 za tumbaku, changanya maji lita nane na uchemshe. Chuja baada ya kupoa, ongeza maji lita nane tena na gramu 60 za sabuni ili kuongeza ubora. Ni muhimu kuwa na tahadhari kwa kuwa tumbaku ni sumu kwa binadamu na wanyama, hivyo weka mbali na wanyama wafugwao. Inashauriwa kuvuna mazao siku 4­5 baada ya kunyunyiza aina hii ya dawa.