KAZI YA MZIZI NA UMUHIMU WA RUTUBA
MMEA: MIZIZI
Mizizi ni sehemu ya mmea ambayo hushikilia mmea ardhini. Pia hufanya kazi ya kunyonya/ kufyonza maji na virutubisho ili kupeleka maji na virutubisho ili kupeleka kwenye shina na majani kutengeneza utomvu ulishao mmea wote.
Utazame mmea ulivyo.
Ng'oa mmea bila kuikata mizizi yake, kwa kuanza kumimina maji mahali ulipoota ili kulainisha udongo. Unapong'oa mmea huu shika karibu na udongo, kama kielelezo kinavyoonyesha.
Ukiangalia mmea huo, Utaona kuna sehemu ya kijani ambayo inakaa juu ya ardhi (Shina na majani) na nyingine ni sehemu ya kijivu ambayo inakaa ardhini (mizizi).
Sehemu iliyo katikati inayotenganisha shina na mizizi inaitwa ukosi; kama vile mkunjo wa kola ya shati.
KAZI YA MZIZI
Mizizi huushilia mmea ardhini
Mara nyingine udongo kwenye mizizi huchukuliwa na maji yaendayo kasi matokeo yake, mimea huanguka na kufa kwa kwasababu mizizi inashindwa kufanya kazi yake.
Iwapo mizizi itashika vema ardhini mmea utaendelea kusimama imara. Udongo unapotifuliwa vizuri mizizi huweza kupenya kwa urahisi ardhini, huwa mingi na kuwa imara. Hivyo maji yaendayo kasi au upepo mkali haviwezi kuung'oa mmea huo kwa urahisi.
Mizizi huupatia mmea chakula
Mizizi hufyonza virutubisho (chumvi chumvi) vilivyoyeyushwa na maji kutoka ardhini na kupeleka kwenye shina na majani kutengeneza utomvu ambao ni chakula cha mmea wote.
Udongo ukiwa na maji na virutubisho vya kutosha, mizizi huupatia mmea chakula cha kutosha. Hivyo mmea hustawi vema zaidi na mkulima hupata mavuno mengi.
Mmea hauwezi kuvipata virutubisho hivi ikiwa hakuna maji ardhini. Hivyo itakuwa jambo la busara kuhakikisha kuwa kuna unyevu wa kutosha shambani.
Tahadhari:
Maji yasisimame juu ya ardhi kwani yatazuia hewa kuingia ardhini. Maeneo yenye maji yaliyosimama hyafai kwa kilimo kwani mizizi huoza. Ila mpunga na miwa inaweza kustawi sehemu zenye maji yaliyosimama.
Ikiwa ardhi itatifuliwa kabla ya mvua za kwanza, mvua zitakaponyesha maji yataweza kuingia ndani ya ardhi. Yataingia bila kupotea na yataifadhiwa. Yatahifadhiwa katika hali ya myeyuko (vurutubisho vilivyoyeyushwa na maji ) ambao utafyonzwa na mzizi ya mimea.
Ukitaka kuwa na mimea yenye afya hakikisha kuna maji ya kutosha pamoja na virutubisho. Hivyo ni muhimu kuitifua ardhi yako kwa njia ifaayo.
UMBILE LA MIZIZI
Utazame kwa makini ule mmea ulioung'oa utaona kuwa mizizi yake imeanza penye ukosi. Mizizi ya mimea aina ya nyasi ni tofauti na ile ya mikunde lakini kazi zake zinafanana.
Mizizi ina matawi mengi madogo madogo ambayo yanaitwa vijizizi. Vijijizizi hivi vipo pembeni mwa mizizi. Tutajifunza zaidi juu ya vijijizi hivi, kwa kuwa ndizo sehemu muhimu kabisa za mizizi ya mmea.
VIJIJIZI
Umbile la vijizizi
Vijizizi navyo vina matawi mengi na madogo sana ambayo si rahisi kuyaona kwa macho tu. Ili kuvipata vijizizi hivi, panda mbegu ya harage ardhini. Iache hapo kwa muda wa siku tatu kisha ifukue kwa uangalifu sana. Mizizi yake itakuwa na urefu kama ule wa njiti ya kiberiti.
Ukitaka kuviona vijizizi hivi vema tumia kioo cha kukuza ukubwa wa vitu (lens). Unaweza kuazima kutoka kwa mwalimu wa shule iliyo karibu na wewe.
Ukivitazama vijizizi kwa makini utaona:
* Kirungu kidogo tena kigumu penye ncha ya kijizizi. Kirungu hiki hukiwezesha kijizizi kupenya ardhini kwa urahisi na kusambaa kama udongo umetifuliwa vizuri.
* Nywele nyingi fupi na nyembamba sana. Nywele hizi huitwa vinyweleo ambavyo hunyonya myeyuko (unyevu) ulioko ardhini.
* Juu zaidi kupita vinyeleo hivi kijizizi huwa kigumu na cheusi zaidi. Hii ndiyo sehemu ya mzizi yenye umri mkubwa kuliko mwingine.
VINYWELEO
Vinywelenywele vilivyoko kwenye vijizizi huwa ni vingi sana vyembamba, vifupi na dhaifu. Vinaitwa vinyweleo.
Vinafanana na nywele za mkono wa binadamu ila ni fupi na nyembamba zaidi.
Vinyweleo hivi hunyonya chakula kinachohitajika na mmea kutoka ardhini huchukua myeyuko wa chumvi chumvi na maji. Ndani ya mmea myeyuko hugeuzwa utomvu unaulisha mmea.
Mmea unastawi, kuishi na kuzaa.
NDANI YA MZIZI
Chukua mzizi mnene kidogo Ukate/upasue kwa kutumia kisu.
Utaona:
* Tabaka ya ganda au gome ambalo ni mfano wa ngozi nyembamba.
* Ndani kidogo ipo tabaka ngumu yenye aina ya maji maji ndipo hapo utomvu hupitia ndani ya virija vidogo ambayo havionekani kwa macho tu.
Virija huusafirisha utomvu mpaka kwenye sehemu zote za mmea. Kazi ya virija vya mmea kusafirisha utomvu, inafanana na kazi ya mishipa ya binadamu kusafirisha damu mwilini.