KUPUMZISHA SHAMBA HUONGEZA RUTUBA ARDHINI

Share:
Mkulima anaweza kuongeza rutuba ardhini kwa kupumzisha shamba lake. Kupumzisha ardhi ni jambo la kawaida. Baada ya kuitumia ardhi kwa kilimo kwa muda wa miaka 3 au 4, mavuno huanza kupungua. Ardhi huwa imechoka. Ndipo inapokuwa busara kuipumzisha.

Kwa nini mazao hupungua
Baada ya miaka 3 au 4 mimea huwa imekwisha nyonya chumvichumvi yote kutoka katika hilo shamba. Pia kiasi cha mboji huwa kimepungua.

Mkulima hutumia busara yake kuamua kutolima ardhi hiyo kwa muda. Kupumzisha ardhi ni jambo la busara.

Ardhi ikipumzishwa huotesha magugu ya aina mbalimbali. mimea hii huuhifadhi udongo usichukuliwe na maji au upepo. Mimea hii itakapokufa, Viini na vijidudu vitaishambulia na kuigeuza kuwa mboji na chumvichumvi. Hapo ardhi hurudiwa na nguvu yake. Umbo lake zuri huonekana tena.

Lakini katika maeneo yenye watu wengi ni vigumu kuipumzisha ardhi kwa muda mrefu. Hakuna ardhi ya kumtosha kila mkulima.

Je tuipumzishe ardhi bila kupanda chochote?
Mkulima wa kisasa anataka ardhi yake irudiwe na ubora katika muda mfupi iwezekanavyo. Hana sababu za kuyaacha magugu yaote ovyo. Wakulima wengine huipumzisha ardhi yao kwa njia bora zaidi ya kisasa.

Shabaha ya mkulima kama huyu ni kuweza kuitumia ardhi hii tena baada ya muda mfupi iwezekanavyo.

Njia ya kisasa ya kupumzisha ardhi itampasa mkulima kufanya kazi zaidi. Lakini kazi hii haitakuwa ya bure kwa kuwa udongo utarudiwa na ubora wake  kwa haraka zaidi.

Jinsi ya kupumzisha Ardhi kisasa.
* Usichome nyasi na majani.
ambayo yameota kwenye ardhi hiyo. Moto huaribu rutuba ardhini. Ardhi kama hiyo hupungua mboji yake.

* Panda mimea.
hasa ile inayoufunika udongo kwa njia bora zaidi. Mimea hii huupa udongo rutuba na kuulinda. Aina nzuri za mimea kama hii ni pamoja na viazi vitamu, malisho ya mifugo kama marejea n.k. Mimea hii huufanya udongo wa shamba lililopumzishwa kuwa bora zaidi.

Mimea hii huifunika ardhi na hutumiwa baadaye kama mbolea ya kijani Baadhi ya mimea hii huweza kutumiwa kama chakula kwa mifugo au watu pia.

Wakati unapowadia mimea hii hufyekwa. kisha hufukiwa ardhini wakati wa kutifua kwa jembe la mkono au plau.

Jinsi ya kufanya ili usihitaji kuipumzisha ardhi mara kwa mara.

Yakupasa uzuie udongo usiwe na ukosefu wa chumvichumvi au mboji.

Utafanyeje
- Tifua udongo kabla ya kupanda.
- Tandaza mabua shambani, yafukie chini wakati unapotifua
- Tandaza nyasi shambani kama ulivyofanya kwa mabua; au tandaza kwenye mashina ya mimea ili kuhifadhi unyevu wa ardhini.
- Tandaza samadi, tifulia ndani ya udongo, samadi itakapooza itaongeza rutuba ya shamba.
- Tumia mbolea ya mchanganyiko kama unavyotumia samadi.
- Tumia udongo wa zizini. Huu nao huongeza utuba unapotandazwa shambani na kutifuliwa kabla ya kulitumia shamba.
- Kilimo cha mzunguko wa mazao. Unapobadili mazao, unawezesha pia kurudishwa kwa rutuba ardhini. Baadhi ya mazao, kwa mfano mikunde, huacha Naitrojeni ardhini.
- Tumia mbolea ya kijani. Mimea kama marejea, majani ya lukina, n.k. uynapotandazwa shambani na kufukiwa wakati wa kutifua hurutubisha udongo.
- Tumia kilimo cha mseto wa mazao tupu au mazao na miti. Njia zote mbili huhifadhi udongo usimomonyoke na kuongeza rutuba shambani.

kadri unavyotumia mbinu zilizotajwa hapo juu kuutubisha shamba lako ndivyo unavyoweza kuendelea kuitumia ardhi hiyo kwa kilimo kwa muda mrefu kabla hujaipumzisha kwa muda mrefu kabla hujaipumzisha tena.