MATUMIZI YA MBOLEA YA SAMADI KATIKA KURUDISHA RUTUBA YA UDONGO
Unaweza kuurudishia udongo rutuba kwa kutumia samadi.
Samadi ni nini?
Samadi ni mchanganyiko wa nyasi, majani na kinyesi cha mifugo, baada ya vyote hivi kuizeshwa pamoja.
Samadi hufaa kwa njia gani?
Samadi inapochanganyikana na udongo huongeza mboji ambayo hulifanya umbo la udongo kuwa bora zaidi. Pia huongeza virutubisho (chumvichumvi). Yote haya huuongezea udongo rutuba inayofaa kuliko njia nyingine zote.
Jinsi ya kutengeneza samadi.
Unaweza kutengeneza samadi ikiwa una mifugo: Ng'ombe, kuku, sungura n.k.
Ukitaka kufanikiwa katika jambo hili usiwaache wanyama wako kuzuzura ovyo. Wajengee banda na uzio. Ndani ya banda hilo tandaza mabua ya mpunga, au mtama au ya mahindi au nyasi kavu, kila mara.
Wanyama watadondosha kinyesi chao juu ya mabua au nyasi ulizotandaza. Viini vilivyoko kwenye kinyesi vitayafanya mabua au nyasi kuoza. Hapa utapata aina safi sana ya mbolea. Samadi ikiwa nyingi kwenye banda iondoe na kuikusanya mahali pa kutolea samadi.
Tumia chombo mfano wa uma kuisukuma. Ukishaondoa samadi yote bandani tandaza nyasi au mabua mapya sakafuni kama ulivyofanya hapo awali
Banda la kuhifadhi mifugo
Shimo au mahali pa kutolea samadi pawe karibu sana na banda. Chimba shimo la kiasi (kulingana na ukubwa wa kundi lako) lenye kina cha nusu mita (futi moja na nusu) Kandokando ya shimo hili chimba mfereji au ikiwezekana jenga ukuta mfupi kuzuia maji yasiingie ndani.
Humo shimoni hifadhi ile samadi yote. Weka mazoea ya watu wa nyumbani kutupa jivu na takataka humo shimoni. Jivu lina chumvichumvi na takatak zimejaa rutuba.
Angalia:
Wasitupe vioo au chupa zilizovunjika, au vipande vya bati au chuma ndani ya shimo. Tkataka hizi zinaweza kuumiza wakati unafanya kazi shamabani.
Samadi ya kuoza isiachwe kukauka. Ikiwezekana mwagilia maji. Maji haya yanaweza kuwa yale yaliyokwisha tumika. Angalia maji hayo yasiwe mengi mno. Ni vema kuikinga samadi ischomwe na jua. Ikiwezekana weka paa ili shimo hilo liwe kivulini. Samadi ili iwe bora ni lazima ibaki shimoni humo ioze kwa muda wa miezi mitatu. Baada ya kipindi hicho ndipo itafaa kupelekwa shamabani
Jinsi ya Kutumia Samadi hii
Muda mfupi kabla hujaanza kulima, au mara baada ya kuchimba mashimo ya kupandikiza miche yake toa samadi na kuipeleka shambani. Kazi hiyo itahitaji mkokoteni au toroli. Kama una ng'ombe au punda unaweza kuwatumia kuvuta mkokoteni huo.
Tandaza samadi hii kote shambani, au iweke ndani ya mashimo utakamopanda miche. Baada ya kufanya hivi tifua shamba, au fukia mashimo uache alama tu.
Unapotumia samadi tumia vipimo vifuatavyo
Kwa ekari moja ya shamba. Mikokoteni 30 au magunia 100 au madebe 500 ya samadi wakati wa kutifua udongo utachanganyika na samadi vema. Udongo utaifunika samadi hiyo Hivyo jua au mvua haviwezi kuiharibu. Samadi hubakia na nguvu yake yote