MBOLEA YA MCHANGANYIKO
Unaweza kuurudishia udongo rutuba kwa kuweka mbolea ya mchanganyiko (mboji). Kama hufugi ng'ombe au mbuzi, au kondoo au punda au nguruwe au kuku, huwezi kutengeneza samadi. Lakini unaweza kutengeneza mbolea ya mchanganyiko.
Mbolea hii ni mchanganyiko wa nyasi, mabua ya mahindi, au ya mtama yaliyokatwa vipande vipande, mboga au matunda yaliyoharibika, jivu, udongo na maji kiasi. Hivi vyote huachwa na kuoza pamoja.
Kama ilivyo samadi, mbolea ya mchanganyiko pia hurudisha rutuba ardhini na kuigeuza kuwa mboji na chumvichumvi.
Jinsi ya kutengeneza mbolea ya mchanganyiko. Chimba shimo lenye kina cha futi mbili karibu na nyumba yako. Ndani ya shimo hili tupa nyasi na masalia ya mazao kutoka shambani. Wajulishe watu wote wa nyumbani juu ya umuhimu wa kuwa na mbolea ya mchanganyiko, na kwamba wote wajenge tabia ya kutupa shimoni humo jivu, na mabaki ya chakula.
Mwaga maji shimoni mara kwa mara ili yaliyomo yapate kuoza. Kumbuka kuwa maji mengi mno huiharibu mbolea yako. Ni vema kama mbolea hivyo itakuwa kivulini, chini ya mti au jenga paa juu ya shimo.
Vile vile chimba mfereji kandokando ya shimo ili maji yanayotiririka yasiingie ndani. Kila mwezi igeuze ili mbolea ya juu iende chini na ya chini iende juu.
Shimo likijaa iache mbolea ioze. Mbolea itakuwa tayari kwa kutumiwa baada ya muda wa miezi miwili mpaka mitatu (2-3).
Jinsi ya kutumia mbolea ya mchanganyiko. Tumia mbolea hii kwa viwango vile vile vya samadi kwa ekari.
"Utajiri wa mkulima mwenye busara ni samadi na mbolea ya mchanganyiko. Hazimgharimu pesa yoyote; lakini thamani yake ni kubwa sana. Hata mkulima mwenye uwezo mdogo kiuzalishaji anaweza kupata mbolea hii."