UBUNIFU: KURUTUBISHA UDONGO KWA KUTUMIA MBOLEA YA ASILI YA MAPAMBANO

Share:
Mbolea ya mapambano ilibuniwa na Bi. Suzana Sylvester, mkulima mbunifu kutoka kijiji cha Haubi, Wilaya ya Kondoa katika Mkoa wa Dodoma Tanzania. Mkoa wa Dodoma hupata msimu wa mvua wa wastani wa milimita 500 hadi 800 kwa mwaka. Hali ya hewa ni ya ukame yenye kipindi kirefu cha jua na mara nyingi hupata mvua zilizopo chini ya kiwango cha wastani. Hali hii inasababisha shughuli za kilimo kuwa ngumu, uzalishaji kuwa mdogo na matukio ya njaa kila mwaka kutokana na kutojitosheleza kwa chakula  katika kaya. Kijiji cha Haubi kimeathiriwa sana na mmomonyoko wa ardhi unaosababishwa na hali unaosababishwa na hali ya aslili ya udongo wake, mvua zisizotabirika, pamoja na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli mbalimbali za binadamu.

Lengo mahsusi la ubunifu                                                                                                                    
Lengo mahsusi la kubuni mbolea ya mapambano ni kuongeza rutuba kwenye udongo, kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo,  kuhifadhi unyevunyevu kwenye udongo na kuboresha udongo kwa kuuongezea mbolea ya mboji  kwa kutumia rasilimali zilizopo zilizopo kijijini Haubi.

Kilichomsukuma kuanza kubuni
B Suzana Sylvester ni mjane mwenye watoto nane. Baada ya kufiwa na mume wake, Bi Suzana alipata changamoto ya kuhudumia peke yake familia kubwa aliyoachiwa na marehemu mume wake kwani hakuwa na kipato chochote cha kumwezesha kupambana na chanagamoto hiyo. Alikaa chini akafikiria njia zote mbadala za kuwezesha kuongeza kipato kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo. Katika kuhangaika, alikumbuka somo alilofundishwa wakati anasoma shule ya msingi enzi za ukoloni, linalohusu njia za kurutubisha udongo kwa kutumia mbolea za asili, utayarishaji wake pamoja na uandaaji wa matuta kwa ajili ya uvunaji maji ya mvua na kuhifadhi unyevunyevu kwenye udongo kwa ajili ya kusta wisha mazao mbalimbali. Baada ya hapo alifanya jaribio la kuandaa mbolea ya asili. Alichimba shimo akalijaza takataka za kila aina. Baada ya miezi 6, alikuwa ameweza kujitengeneza mbolea nzuri ya mboji yenye rutuba ya kutosheleza shamba lake la ekari tatu. Baada ya kutumia mbolea hiyo katika shamba lake, uhai wa shamba lake uliongezeka na mavuno yakaongezeka kwa kiasi kikubwa. Baada ya kuona matokeo mazuri na kupunguza changamoto alizokuwa nazo, aligundua kwamba mbolea hiyo ndiyo mkombozi katika changamoto zilizokuwa zikimkabili na hivyo akaamua kuipa jina la Mapambano.

Maelezo mafupi juu ya ubunifu huu
Katika kuandaa mbolea ya mapambano, shaghuli ya kwanza ni kuchimba shimo la mita 3 urefu kwenda chini na mita 2.5 upana. Baada ya kuchimba shimo, unatanguliza majivu chini kama futi moja. Juu ya majivu unaweka majani na takataka za kila aina , mkojo wa mifugo, maji machafu ya jikoni, majani makavu na uchafu wote wa nyumbani mpaka shimo lijae. Shimo linatakiwa kujaa hadi kufikia nusu futi juu ya usawa wa ardhi. Shimo likisha jaa, unafunika taktaka hizo kwa majivu yakifuatiwa na majani. Shimo hilo linaendelea kumwagiliwa kwa kutumia maji machafu ya nyumbani kwa ajili ya kuhifadhi unyevunyevu. Baada ya miezi 5 hadi 6 mbolea huwa tayari kwa kupeleka shambani kurutubisha udongo. Wakati wa kupanda mazao. Kipimo cha mbolea ya Mapambano kinachotumika ni kwa kiwango cha 1/4 hadi 1/2 kilo katika shimo moja la kupanda mazao.

Faida alizozipata kutokana na Mbolea ya mapambano
- Kuongeza uzalishaji kwenye eneo kutoka gunia 3 hadi gunia 20 za mahindi katika ekari moja
- Kuongeza kipato kutokana na mauzo ya mazao ya ziada, kujitosheleza kwa chakula na kuondokana na njaa ya mara kwa mara.
- Mbolea ya mapambano imemsaidia Bi Suzana Svlvester kuthaminiwa na wakulima wenzake, kufahamika katika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi hasa katika taasisi za utafiti na maendeleo Bi Suzana ameweza kusomesha watoto wake wote, kujenga  nyumba bora, kununua ng'ombe wa maziwa kwa ajili ya kuboresha lishe ya watoto, na kukidhi mahitaji mbalimbali ya msingi
- Amefanikiwa kuongeza rutuba ya udongona kuboresha shamba lake
- Kupitia ubunifu wake ameweza kuunganishwa na kufahamiana na wabunifu wengine ndani na nje ya Mkoa wa Dodoma