JINSI YA KULIMA KWA MKONO

Share:

Chombo kinachotumika zaidi wakati wa kulima kwa mkono ni jembe la chuma bapa, au beleshi la kawaida, au jembe lenye meno mfano wa uma.

Kulima kwa jembe la mkono
Yapo majembe ya aina nyingi na maumbo mbalimbali. Kila sehemu ina aina ya jembe wakulima waliyoizoea zaidi.

Ukitaka kulima vema kwa jembe hili, chagua jembe zito kiasi cha kutosha. Mkulima hodari huchagua jembe lifaalo. Ukiweka chuma cha jembe hili chini mpini wake uonekane umesimama wima.

Ni jambo la muhimu sana kuwa jembe lipenye ardhini vema. Ikiwa chuma cha jembe hakina umbo zuri, kwa mfano, kama kinafanana na ndoana, hakitapenya ardhini itakiwavyo. Utapapasa ardhi juu juu tu badala ya kulima kwa makini.

Jembe la sura ya ndoanaa kwa kupalilia lakini halifai kwa kutifua.

Kulima kwa makini kwa kutumia jembe la mkono kwahitaji chuma cha jembe kupenya ardhini vema. Haifai kuukwaruza udongo juu juu tu kwa jembe kama vile wakulima wengine wafanyavyo.

Unaweza kuweka samadi, nyasi au masalia ya mazao kwenye mtaro unapolima.

Unapoanza kulima fanya hivi:
Ikate ardhi kwa jembe lako, kisha livute jembe upande uliko. Jembe litauleta udongo miguuni pako. Udongo huo utaifunika takataka yoyote hapo.

Kama bonge la ardhi ni kubwa mno, tumia kisogo cha jembe kulivunja bonge hilo. Ukitifua ardhi yako namna hii kwa muda wa miaka 3 au 4 hivi, utalibadili kabisa umbo la udongo wako. Udongo utakuwa na nguvu zaidi na mimea yako itastawi vema zaidi.

Ukilima shamba lako namna hii kila mwaka kazi ya kulima itakuwa rahisi sana. Hutachoka sana hasa kama unazifukia takataka ardhini.