KILIMO CHA MIGAZI

Share:

Migazi au michikichi ni mimea aina ya mitende inayostawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba nyingi na uisojaa maji wakati wote. Mimea hiyo hupenda pia mvua nyingi. Matunda ya migazi au michikichi hutoa mafuta yanayoitwa mawese. Mafuta ya mawese yana rangi ya manjano na hutumika kwa kuungia aina mbalimbali za mboga za majani, maharage  au aina mbalimbali za kitoweo.

Aina za migazi
Kuna aina kuu tatu za migazi. Dura ambayo ina mbegu kubwa iliyozungukwa na nyama nyembamba. Aina hii hutoa mafuta kidogo kulinganisha na zingine. Aina ya pili ni Tenera ambayo ina mbegu ndogo inayozungukwa na nyama nyingi, aina hiyo hutoa mafuta mengi. Aina ya tatu ni chotara wa Dura na Tenera. Aina hiyo hutoa mafuta ya kadiri

UKUZAJI WA MIGAZI
Migazi huweza kukuzwa kwa kupanda kwenye kitalu au moja kwa moja shambani

Kupanda kwenye kitalu
Mbegu za migazi huoteshwa kwanza kwenye kitalu. Katika kitalu matuta yanaweza kuwa na upana wa mita moja na urefu wowote kulingana na hali ya ardhi. Matuta hayo yadidimizwe chini ya ardhi kama ufa kwa sentimeta tano. Mbegu ipandwe katika mistari kwa nafasi ya sentimenta 45 kwa 60 kati ya mche na mstari. Mbegu huchukua wiki tatu hadi nne kuchipua. Miche uhamishiwa shambani ikiwa na urefu wa sentimita 25 ahdi 30.

Kupanda katika shamba
Safisha shamba na kuondoa magugu yote. Tayarisha mashimo ya kina cha sentimeta 60 na upana wa sentimeta 60. Tenga udongo wa juu na wa chini wakati wa kuchimba shimo. Changanya udongo wa juu na debe moja la samadi au mboji na kurudishia shimoni. Hakikisha kuwa shimo linajaa udongo uliochanganywa na samadi au mboji. Pandikiza miche yako baada ya wiki mbili.

Migazi hupandwa kwa nafasi ya mita 10 kwa mita 10. Unaweza kupanda mazao mengine kama vile kunde, muhogo na viazi vitamu katika shamba la migazi. Miche ya migazi ipandikizwe wakati wa masika au wakati wowote endapo shamba lina unyevu wa kutosha.

KUTUNZA SHAMBA
Migazi ipaliliwe mara magugu yaonekanapo shambani. Wakati wote shamba liwe safi ili kuiwezesha mimea kukua vizuri na kuepukana na athari ya miche kuungua na moto.

Mbolea
Mbolea aina ya chumvi chumvi inaweza kutumika katika kukuzia migazi kwa miaka miwili hadi tatu ya mwanzo. Mboji inaweza kutumika pia katika kurutubisha migazi katika umri wowote.

Magonjwa na wadudu waharibifu
Migazi ni zao ambalo halina magonjwa muhimu sana. Kwa hali hiyo halihitaji mbinu maalum ya kuzuia na kutibu magonjwa. Mchwa ni aina ya wadudu wanaoshambulia sana migazi sehemu ya ardhini. Mashambulizi hayo yanaweza kuua mmea mzima. Ili kuzuia mchwa unaweza ukaloweka mizizi na sehemu ya shina la mmea katika dawa ya Aldrin.

Wakati wa kupanda unaweza ukamwagia pia dawa aina ya Gaumalin kwenye udongo unaozunguka mgazi.

KUVUNA NA HIFADHI
Mgazi huanza kuzaa ukiwa na miaka 3-4 kutegemeana na aina yake. Mgazi mmoja unaweza kutoa mikungu 8-9 kwa mwaka yenye uzito kati ya kilo 40-50. Mti mmoja unaweza kutoa lita 40.5 za mafuta ya awese kwa mwaka. Matunda ya migazi yaanguliwe yakishaiva na kuonyesha rangi ya manjano.

Toa matunda ya migazi kutoka kwenye mikungu na chemsha kwa muda hadi kuiva. Epua na kuyatwanga kwa kutumia kinu kama unavyokoboa mahindi. Toa mashudu na kuyaweka ndani ya sufuria yenye maji na chemsha tena, kamua mashudu na kuyatupa. Maji na mawase yatabaki kwenye sufuria. Katika kuendelea kuchemsha, mawese yatajitenga na maji na kutanda juu ya maji. Engua mawese taratibu hadi kwisha.

Weka mawese ndani ya sufuria na uyapashe moto ili kuyakausha. Hifadhi mawese ndani ya chupa, debe au pipa safi na funika vizuri.

Kumbuka
Matunda ya migazi yakiiva sana au yakiharibika (kuoza) hutoa mafuta yenye kukereketa kooni. Pia matunda yakiwa ambichi hayatoi mafuta mengi.