Viazi ni zao ambalo hulimwa katika sehemu nyingi za Tanzania. majani ya viazi yana wingi wa vitamini A, C, chuma na chokaa. Viazi huliwa kwa kuchomwa, kukaangwa au kuchemshwa. Majani yake hutumika kama mboga (matembele).
AINA YA VIAZI
Viazi vitamu vipo vya aina nyingi kama vile, vya rangi ya manjano, nyeupe, nyekundu n.k, lakini vyenye vitamini A kwa wingi ni vile vya rangi ya manjano. Viazi vina vitamini C kwa wingi pia.
NAMNA YA KUTAYARISHA BUSTANJI
Udongo unaofaa kwa kilimo cha viazi vitamu ni wa kichanga, wenye rutuba na usiotuamisha maji. Viazi hupandwa katika sesa au matuta. Kilimo cha matuta ni bora kwa sababu huzuia mmonyoko wa udongo, huhifadhi unyevu na huahisisha uvunaji. Hali kadhalika mavuno huwa bora na mengi zaidi.
Tayarisha shamba mapema, kabla mvua hazijaanza kunyesha. Iwapo utapanda viazi kwenye matuta, tengeneza matuta yenye mwinuko wa sentimita 30 hadi 50. Weka mbolea ya samadi au mboji mwezi mmoja kabla ya kupanda. Katika sehemu za mwinuko tayarisha matuta kukinga mteremko.
KUPANDA
Viazi vitamu hupandwa kwa kutumia pingili zenye urefu wa sentimita 20 hadi 45. Chagua pingili zenye macho mengi na zisizo na dalili za magonjwa au wadudu.
Ziache pingili zinyauke kwa muda wa siku moja hadi mbili kabla ya kupanda. Panda katika nafasi ya sentimita 15 hadi 60 kwa mmea hadi mmea na sentimita 90 kati ya tuta na tuta. Wakati wa kupanda fukia nusu ya pingili. Pingili zipandwe kwa mshazari na sio wima.
MATUNZO YA BUSTANI
Palizi
Palilia bustani mara magugu yanapoota. Wakati wa kupalilia pandisha udongo.
Magonjwa na wadudu waharibifu
Viazi hushambuliwa zaidi na magonjwa yatokanayo na virusi ambavyo husambazwa na inzi weupe. majani yaliyoshambuliwa na ugonjwa huo, huwa na rangi nyupe na hujikunja, hatimaye hudondoka kwa urahisi. Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia usafi wa shamba na kupanda mazao kwa mzunguko.
Magonjwa mengine ni pamoja na yale yanayosababisha viazi kuoza. Ili kuepukana na magonjwa haya:
- Tumia mbegu ambazo hazina dalili za magonjwa haya;
- Viazi vinavyoonyesha dalili ya kuoza viondoe na uvitupe.
Wadudu
Wadudu wanaoshambulia viazi ni minyoo fundo (nematodes) na bungua (sweet potato weavil)
Minyoo fundo
Hushambulia viazi na kusababisha viwe na umbo lisilo la kawaida.
Bungua
Hushambulia majani na viazi, hivyo husababisha majani kunyauka na viazi kuoza. Zuia wadudu hawa kwa kuweka shamba katika hali ya usafi, vuna mapema na panda kwa mzunguko. Dawa kama malathion pia inaweza kutumika katika kuzuia uharibifu wa wadudu hawa.
Wanyama waharibifu
Viazi vitamu husahmbuliwa na wanyama kama panya, fuko, ngedere na nguruwe. Zuia uharibifu wa wanyama hawa kwa kawawinda, kutumia mitego na kuweka eneo linalozunguka bustani katika hali ya usafi. Wanyama wengine ni mbuzi na ng'ombe. Ikiwezekana ua kwenye eneo la bustani.
KUVUNA NA HIFADHI
Vuna majani ya viazi yangali machanga kwa ajili ya mboga. Viazi huwa tayari kuvunwa baada ya miezi mitatu hadi minne kutegemea na aina ya viazi na mahali. Vuna kwa uangalifu ili kuhakikisha viazi havipati mikwaruzo au majeraha.
Majani yakaushwe kwa kutumia njia bora ili kuzuia upotevu wa vitamini A. Hii ni pamoja na kutumia kaushio, kuanika kivulini au kufunika mboga kwa kutumia kitambaa au plastiki nyeusi. Viazi vinaweza kuhifadhiwa kwa njia zifuatazo:
Kufunika viazi chini
- Baada ya kuvuna, chagua viazi ambavyo havina mikwaruzo, michubuko au majeraha;
- Weka viazi hivi kwenye shimo lililotandazwa majani makavu, funika na majani. Kisha fukia kwa udongo. Njia hii inaweza kuhifadhi viazi kwa muda wa siku 28.
Kukausha viazi
Baada ya kuvuna viazi, vioshe, vimenye kisha anika na hifadhi kwenye debe, chungu au kihenge. Viazi pia vinaweza kuchemshwa kabla ya kukaushwa. Kaushio linaweza kutumika kuharakisha ukaushaji na kupunguza uharibifu wa vitamini A