KULIMA KWA PLAU

Share:

Katika nchi yetu, wakulima wengi wameshazoea kutumia ng'ombe au punda kukokota plau au mkokoteni. Wanafurahi uzoefu huo kwa sababu wameshapata faida nyingi. Wakulima wengine bado wanasitasita kutumia ng'ombe wao kufanya kazi.

Kweli faida za kilimo cha ng'ombe ni nyingi ukilinganisha na kilimo cha jembe la mkono
- hurahisisha kazi. Mkulima hachoki.
- Mkulima anaweza kulima eneo kubwa zaidi.
- Kazi ya kupalilia itakuwa rahisi zaidi.
- Kutifua udongo kunafanyika vizuri zaidi yaani plau hupindua udongo vizuri, hufukia vizuri samadi, nyasi na majani, hulainisha ardhi.
- Plau husaidia kurutubisha ardhi zaidi

PLAU YENYEWE
- Sehemu zote zimefungwa kwenye fremu.
- Kisu hukata udongo.
- Chuma mfano wa ulimi hupindua udongo.
- Kisigino huwezesha plau isimame wima.
- Mnyororo hufungwa kwenye fremu.
- Gurudumu hurekebisha kina cha mfereji.
- Kirekebisho hurekebisha upana wa mfereji
- Mikono 2 hutumika kuongoza plau

JINSI YA KUIREKEBISHA PLAU
Upande wa mbele wa plau zipo sehemu za kuirekebisha plau yako. Yaani kulima vizuri shambani kwako kufuatana na hali ya ardhi.

Gurudumu:
Hili hukuwezesha kulima kwa kina fulani. Ukilisukuma juu gurudumu hili kina kitakacholimwa kitakuwa kikubwa zaidi. Ukilirudisha chini, kina kitapungua.

Kirekebisho:
Hiki hukuonyesha upana wa udongo utakaokatwa na kisu cha plau yako. Hiki hukuwezesha kuisogeza ndoana ya plau. Ukitaka kisu kikate sehemu pana zaidi isogeze ndoana kuelekea upande uliolimwa. Ukitaka kisu kikate sehemu nyembamba zaidi isiogeze ndoana upande ambao haujalimwa.

Kirekebisho hutumika pia kuiwezesha plau isimame wima. Kisu na kisigino vikae sawa katika mfereji