Maelekezo ya Mvua za Vuli Oktoba mpaka Disemba 2018

Share:
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2018, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbali mbali wanaohitaji taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na 

Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Uchukuzi na  Mawasiliano, Nishati na Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa
Mvua za vuli, zinazonyesha kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki, Ukanda wa Pwani ya kaskazini na wilaya ya Kibondo). Mvua za Vuli 2018 zinatarajiwa kuanza mapema katikati ya mwezi Septemba na mwanzoni mwa Oktoba, 2018 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo; mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na maeneo ya mashariki na kusini mwa Ziwa Viktoria. Mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya pwani ya kaskazini.
Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga):
Mvua za vuli zinatarajiwa kuanza mapema, kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Septemba, 2018 katika maeneo ya mkoa wa Mara na kusambaa katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita na Kagera ifikapo wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2018. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu. Mvua za wastani na vipindi vya mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo. Mvua za msimu wa Vuli zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2018 katika maeneo ya mikoa ya Mara na Simiyu, na kwa maeneo mengine ya ukanda wa Ziwa Viktoria mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari, 2019
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2018. Mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi. Vipindi vya ongezeko la mvua vinatarajiwa hususan katika ya miezi ya Oktoba na Novemba. Mvua za Vuli zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu ya mwezi Disemba, 2018.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na
Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2018 na
zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Disemba, 2018.