UFUGAJI BORA WA KAMBALE

Share:

Kambale (Ietalurus Punetaus), ni aina ya samaki ambao wana majina mengi kulingana na eneo na jamii husika. Samaki hawa unaweza kusikia wakitajwa kwa majina mengine kama vile, kambale channel, koleo, samaki kidevu Na kuendelea.

      Asili ya Kambale
Asili ya samaki hawa ni Amerika ya Kaskazini. Samaki hawa hukua kwa haraka sana, na kuwa na uzito mkubwa. Aina hii ya samaki hupendwa na watu wengi kwa kuwa nyama yake ina ladha nzuri na ni laini sana.

Samaki hawa huzaliana vizuri zaidi wanapokuwa mtoni au sehemu ambayo wanapata tope. Mfugaji anapokusudia kufuga aina hii ya samaki kibiashara, ni lazima kusakafia bwawa ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababishwa na samaki hawa.


      Umbile lake
Samaki aina ya kambale wana umbo refu, pia ni wapana kuanzia shingoni, ingawa kichwa ni kidogo, na upande wa mkia ni mwembamba. Samaki hawa wana rangi ya kijivu na wengine nyeusi.


Jinsi ya kulisha kambale
Unaweza kulisha kambale kwa kutumia unga wa samaki, maharagwe yaliyosagwa, mahindi, mchele pumba, ngano na bidhaa nyingine. Unaweza kujenga mfumo ambao utawawezesha samaki hawa kupata aina mbalimbali za wadudu, pamoja na majani, ili kusaidia wapate mlo kamili.


      Ukuaji na uvunaji wa kambale
Aina hii ya samaki, wakitunzwa vizuri, wanaweza kukua kwa haraka na kuwa na uzito mzuri unaoweza kumpatia mfugaji faida nzuri. Unaweza kuanza kuvuna kambale baada ya miezi sita tangu walipopandikizwa kwenye bwawa.

Mambo ya kuzingatia kabla ya kufuga samaki
Fahamu ni aina gani ya samaki inayopendwa zaidi katika eneo ulipo.
- Samaki wanaopendwa wanatakiwa wawe na ukubwa gani.
- Kiasi cha samaki kinachohitajika katika soko ulipo.
- Ni kipindi gani ni kizuri kwa uvunaji wa samaki.
- Ni wakati gani mzuri wa kuuza samaki.
- Je, katika eneo lako kuna mfugaji mwingine anaezalisha samaki kwa ajili ya soko hilo?.
- Bei ya aina ya samaki unaozalisha ikoje?