NAMNA YA KULIMA MCHICHA

Share:
Mchicha ni mboga za majani ambazo zina faida lukuki katika miili yetu. Kilimo hiki ni kizuri kwa sababu huwa hakichukui muda mwingi katika upandaji hadi uvunaji.

HALI YA HEWA NA UDONGO
Mchicha unahitaji maji ya kutosha katika kipindi chake chote cha ukuaji hadi kuvuna. Vilevile mchicha huhitaji udongo wenye rutuba ya kutosha na wenye kuhifadhi maji.

UTAYARISHAJI
Tengeneza shamba la mchicha kwa kutifua ardhi na kulainisha udongo wenye kina cha sentimeta thelathini. Weka mbolea ya samadi debe moja katika kila mita moja ya mraba. Panda mchicha katika matuta yenye upana wa 90cm-100cm.

AINA ZA MBEGU
- Amarantus africana ni mchicha wenye majani ya kijani na mbegu zake ni ni nyeusi.
- Amaranthus dubius ni mchicha wa kienyeji na Aspinosus ni mchicha wenye miba mingi.
- Amarantus africana ni mchicha wenye majani ya kijani na mbegu zake ni ni nyeusi.
- Amaranthus hybridus huu ni mchicha wenye majani mekundu na mbegu zake ni nyeusi.

UPANDAJI
- Mchicha upandwe katika tuta kwa mistari yenye nafasi ya sentimita thelathini.
- Funika mbegu kwa kutumia udongo uliolaini na tandaza nyasi kavu baada ya kupanda ili kutunza unyevunyevu na toa matandazo baada ya siku tatu hadi tano tangu siku ya kupanda.
- Pandikiza mchicha kwa nafasi ya sentimeta kumi na tano kwa ishirini.
- Mwagilia maji ya kutosha.

MBOLEA
Tumia mbolea ya samadi iliyolowekwa kwenye maji kwa muda wa masaa ishirini na nne kumwagilia mchicha wako ili kupata mavuno mengi zaidi. Tumia kiasi cha debe moja kwa kila mita moja ya mraba.

NAMNA YA KUDHIBITI WADUDU
Adui mkubwa wa mchicha ni wadudu aina ya mafuta au kitaalamu zaidi huitwa spinach aphids ambao hufyonza utomvu wa mchicha na kusababisha majani kujikunja , mchicha kusinyaa na kunyauka. Kudhibiti wadudu hawa mwagilia mchicha wako kutumia chombo kinachotoa maji mithili ya mvua kitaalamu kinaitwa "watering can" ili kuwadondosha wadudu hao.

Wadudu wengine ni kitambazi ambacho hula majani ndani kwa ndani hivyo tumia mwarobani kunyunyuzia majani ili kuwaua wadudu hao waharibifu.

Mavuno
Mchicha huwa tayari kuvunwa baada ya majuma 3 hadi 6 tangu kupandwa au kupandikizwa. Uvunaji huweza kuendelea kwa muda wa miezi 2 hadi 3 kutegemeana na namna utakavyoamua kuuvuna mchicha wako

NAMNA YA KUHIFADHI MCHICHA
         - Vuna mchicha wako kisha usafishe vizuri

    - Funga katika mafungu.
    - Chemsha maji mpaka yachemke.
    - Tumbukiza mafungu ya mchicha katika maji yanayochemka kwa muda wa dakika 1 hadi 2.
    - Kausha vizuri chini ya kivuli na utunze mchicha wako katika sehemu isiyo na unyevunyevu.