KILIMO HAI CHA KARANGA

Share:



Karanga ni moja ya jamii ya kunde, Karanga ni zao maarufu sana duniani katika kilimo cha mzungunguko.

Mmea wa karanga ni moja ya mimea mifupi ambayo huota na kuwa na urefu wa sentimita 15-60 kwenda juu. Matunda yake huwa na kati ya mbegu moja mpaka tano, ambapo viriba vyake huwa chini ya ardhi. Mbegu zake huwa na kiasi kikubwa cha mafuta (38% – 50%), protini, kalishamu, potashiamu, fosiforasi, magnesiamu na vitamini. Inasadikiwa kuwa karanga pia zina aina fulani ya viini vinavyotumika kama dawa.

Hali ya hewa kwa ajili ya kilimo hiki.
Karanga hulimwa kwenye sehemu yenye joto, wastani wa mwinuko wa mita 1500 kutoka usawa wa bahari. Kiwango cha joto kinachohitajika kila siku ni kiasi cha jotoridi 30, na wakati wa ukuaji kinaweza kupungua mpaka jotoridi 15. Hali ya ubaridi huchelewesha karanga kuchanua.

Udongo na kiwango cha maji
Kwa kuwa viriba vya karanga huwa kwenye udongo na ni lazima kuchimbuliwa wakati wa mavuno, huku vikiwa ni vyepesi kuvunjika, ni vizuri kuwa na udongo mkavu, lakini mmea hukua na kustawi vizuri kwenye udongo wa mfinyanzi uliochanganyika na kichanga!

Mvua
Kiasi cha milimita 500-600 cha maji katika msimu wote wa ukuaji wa karanga kinatoa fursa nzuri ya uzalishaji. Hata hivyo karanga ni moja ya mazao yanayostahimili ukame, na linaweza kuvumiliwa ukosefu mkubwa wa maji. Hali inapokuwa hivyo hupunguza kiasi cha mavuno.

Kuna aina mbili za karanga:
Aina ya mafungu
- Aina inayotawanyika

Matunzo
Ili kuwa na mavuno ya hali ya juu, ni lazima magugu yadhibitiwe kabisa. Karanga ni dhaifu sana katika kukabiliana na magugu hasa katika kipindi cha mwanzo cha ukuaji. Ni lazima palizi ifanyike mapema wakati huo miche ikiwa inachomoza kwenye udongo. Miche ikashachomoza palizi ifanyike kwa mikono ili kuepuka usumbufu kwa karanga changa au kuharibu maua.

Palizi ya kawaida inaweza kufanyika mpaka kwenye kipindi cha wiki 6 na palizi ya mikono ifanyike baada ya hapo.

Virutubisho pekee vinavyohitajika kwenye shamba la karanga ni kalishamu. Kalishamu hunyonywa moja kwa moja na viriba vya karanga endapo udongo una unyevu unyevu. Kama kutakuwepo upungufu wa kalishamu, viriba vya karanga vitakuwa vitupu bila kuwa na karanga. Mimea inayohitaji Naitrojeni inaweza kupatikana kwa kushirikisha mimea mingine kama vile kunde, badala ya kuweka mbolea ya Naitrojeni kwenye udongo.


Mavuno
Karanga zinazokomaa kwa muda mfupi zinaweza kuvunwa kati ya siku 85-100 tangu kupandwa, na zinazochukua muda mrefu zinaweza kuvunwa katika kipindi cha siku 110-130 tangu kupandwa. Ng’oa mashina machache kuona kama karanga zimeshakomaa. Karanga zilizokomaa ni lazima ziwe na rangi ya kahawia kwa nje, ngumu na zilizokauka.

Kwa kawaida karanga zilizokomaa ndani ya kiriba huwa na rangi ya kahawia, na hutoa sauti inapotikiswa. Magonjwa yanaposhambilia majani ya karanga yanaweza kusababisha karanga kuvunwa kabla hazijakomaa sawa sawa. Ni lazima karanga zichimbwe kwa umakini ili kuepuka karanga kupasuka na kubakia ardhini.

Anika kwa siku 2-3, kisha zikwanyue na uanike tena kwenye jamvi kwa siku 7-10 ili kuondoa unyevu kufikia asilimia kumi.

Ubambuaji wa karanga ufanyike kwa mikono au kwa mashine maalum. Karanga zilizopondeka, chafu au kuharibika zitengwe kwani zitapunguza ubora wa karanga na kupunguza bei ya kuuzia.

Endapo karanga hazikuhifadhiwa vizuri zinaweza kushika unyevu unyevu ambao husababisha sumu inayojulikana kama aflatoxin ambayo ni hatari sana kwa afya ya binadamu hasa ini. Karanga ambazo zitatumika kwa ajili ya kupanda (mbegu) msimu unaofuata zisibambuliwe kutoka kwenye viriba.