NAMNA YA KULIMA KUNDE

Share:

Kunde ni zao ambalo linaweza kulimwa kwa ajili ya chakula na biashara, pia ni zao lenye kiasi kukubwa cha protini na majani yake yanaweza kutumika kama mboga za majani. Vilevile ni zao ambalo linatoa mavuno ya Kiasi cha kilogram 500 hadi 1500 kwa ekari.

Hali ya hewa
Ni zao linalostahimili ukame, Kunde hukubari vizuri katika mwinuko wa mita 0 hadi 1500 kutoka usawa wa bahari. kunde huweza kulimwa katika maeneo yapatayo mvua kidogo kiasi cha milimita 500 hadi 1200 kwa mwaka. Lakini pia kunde hukuwa vizuri katika joto la nyuzi 28 had 32 C.

Ardi
Huweza kulimwa katika udongo usiotuamisha maji wa aina tofauti tofauti kuanzia kichanga hadi mfinyazi.

Kunde zinaweza kupandwa katika udongo usio na rutuba ya kutosha lakini hustawi vizuri katika udongo wa tifutifu kichanga au mfinyanzi au mchanganyiko wa mfinyazi na kichanga wenye p.H kati ya 6 hadi 7.

Maandalizi ya shamba
Shamba la kunde liandaliwe mapema kabla shughuli ya upandaji kuanza, Kama ni la kukata miti mikubwa miti ikatwe mapema, Kama ni la kufyeka nyasi na miti midogo shughuli hii ifanyike mapema kabla hatua ya kulimwa kwa shamba kwa kutumia trekta, Pawatilla, jembe la ng'ombe au la mikono. Shamba lisawazishwe na kukusanywa mabaki ya mimea au visiki na mawe madogomadogo kama yapo.

Mbegu bora za kunde
Kuna aina mbalimbali za mbegu bora za kunde ambazo zimegawanyika katika makundi makubwa mawili ambazo ni;
- Kunde zinazosimama
- kunde zinazotambaa

BAADHI YA MBEGU BORA NA SIFA ZAKE
Hukomaa kwa muda wa siku 75 – 90. Aina hii ya kunde husambaa ina maua yenye rangi za zambarau na mbegu zake ni mviringo. Maeneo yanayoshauriwa kupanda ni yenye mwinuko wa mita 0 – 1500 toka usawa wa bahari. Inahitaji udongo mwepesi wenye rutuba na usiotuamisha maji. Kunde hizi hutoa mazao hadi tani 3 (kilogram 600 - 1500 kwa ekari)kwa hekta moja. Huvumilia virusi vya mozaiki vinavyotokana na wadudu mafuta wa kunde na bakiteria. Aina hii ya kunde ilizalishwa mwaka 1992 na Kituoa cha Utafiti cha Ilonga kwa ushirikiano na Naliendele.
FAHARI
Aina hii hukomaa kwa siku kati ya 75 – 90. Mmea husambaa na maua yana rangi ya zambarau. Mbegu zake ni za mviringo. Hustawi maeneo yenye mwinuko wa mita 0 – 1500 kutoka usawa wa bahari. Hutoa hadi tani 3 kwa hekta moja (kilogram 600 - 1500 kwa ekari ). Huvumilia magonjwa ya CABMV na mabaka. Fahari ilitolewa mwaka 1982 na Kituo cha Utafiti Ilonga kwa kushirikiana na Naliendele.

VULI_1
Inakomaa kwa siku 55 – 65. Hukua ka kunyooka na kusambaa kidogo. Mbegu zake ni nyekundu na za mviringo. Inastawi vizuri maeneo yenye mwinuko wa mita 0 – 1500 toka usawa wa bahari. Ikipataiwa matunzo mazuri huto hadi tani 2 kwa hekta moja (Kilogram 450-800 kwa ekari). Vuli – 1 inavumilia CABMV, BP na BB Vuli – 1 ilizalishwa mwaka 1987 kutoka kituo cha utafiti Ilonga.

VULI_2
Inakomaa baada ya siku 65 – 70 baada ya kupandwa inaota ikiwa imenyooka na kusambaa kidogo. Mbegu zake zina weupe uliofifia na ni mviringo. Aina hii husitawi vizuri maeneo yenye mwinuko wa mita 0 – 1500 kutoka usawa wa bahari. Katika matunzo mazuri aina hii huzalisha hadi tani 3.5 kwa hekta moja(Kilogram 800 -1200 kwa ekari) . Vuli – 2 huvumilia CABMV, BP na BB Vuli – 2 ilizalishwa mwaka 1987 kutoka kituo cha utafiti Ilonga.

Kupanda kunde.
Kunde hupandwa mwishoni mwa msimu wa mvua ili kuziepusha kukauka wakati mvua inaendelea kunyesha, pia unaweza kupanda wakati zao jingine linakaribia kuvunwa au katika shamba lililovunwa mpunga na lina unyevu wa kutosha. Muda mzuri wa kupanda kunde ni kuanzia mwezi Februari mwishoni hadi Machi na Aprili kwa maeneo ambayo mvua huchelewa kuisha.

KUMBUKA
mbegu zinazotambaa za kunde zipandwe miezi miwili kabla ya mvua kuisha kwani hizi huchukua siku nyingi kukomaa na Mbegu zinazosimama zipandwe mwezi mmoja kabla ya mvua kuisha.

Kunde huitaji kiasi cha kilogram 4-12 za mbegu kwa ekari. kiasi cha mbegu kitategemea ukubwa wa mbegu,(mbegu kubwa zitahitajika kilogram nyingi) nafasi za upandaji,Ukipanda karibu karibu na mbegu itahitajika nyingi, Ubora wa mbegu katika uotaji. Zisizoota vizuri huitaji mbegu nyingi zaidi.

Nafasi ya upandaji.
Unaweza kutumia nafasi zifuatazo kwa kupanda kunde zako.

KUNDE ZINASOSIMAMA
Tumia sentimeta 45 hadi 50 mstari hadi msatari na sentimeta 15 hadi 20 shina hadi shina katika mstari / Sm ( 50 X 20 )

KUNDE ZINAZOSAMBAA
Tumia nafasi ya Sentimeta 70 hadi 75 mstari hadi mstari Kwa sentimeta 25 hadi 30 shina hadi shina katika mstari / Sm ( 75 X 30 ).
Panda kwa kufikia kiasi cha sentimeta 2.5 hadi 5 ardhini na tumia mbegu tatu kwa kila shimo na baadaye punguza uache 2 kwa kila shimo kama unauhakika wa mbegu zako unaweza kupanda moja kwa moja mbili mbili kwa shimo.

Palizi
Palilia na Punguza mimea mapema katika shamba lako la kunde ili ikuwe ikiwa na afya bora.

Mbolea
Kama shamba lako halina rutuba ya kutosha unaweza kuongeza samadi kiasi cha tani tano kwa ekari moja na uhakikishe mbolea hii imemwagiwa au imenyeshewa na mvua ya kutosha kuiozesha kabla ya kupanda kunde zako

Wadudu na magonjwa.
Wadudu waharibifu wa zao la Kunde wako katika makundi mawili:-
- Kundi la kwanza ni la wadudu wanaoshambulia mimea ikiwa shambani. Ina maana mmea hushambuliwa baada ya kuona hali inapokomaa na kutoa mbegu. Kundi la wadudu hawa lina tabia ya kufyonza (Sap = supu) ya mmea kwenye majani, matawi, mashina, maua hata mbegu hasa zikiwa changa kama vitunda.


Njia hii ndiyo pekee kwa wadudu wa kundi hili kujipatia mlo ili waishi na kuzaliana. Katika kundi la pili kuna wadudu wenye tabia ya kukata mashina na kuangusha mimea michanga na wengine hutafuna majani na maua. Zaidi ya uharibifu katika kula mimea, wadudu wengi ni hifadhi ya viini vya magonjwa ya virusi.

- Kundi la pili ni la wadudu waharibifu baada ya mavuno kuwekwa ghalani. Athari ya wadudu hawa inapelekea wakulima kupoteza chakula ghalani pia kupunguza chakula ghalani pia kupunguza ubora wa mazao yanapopelekwa sokoni mfano Mahindi yanapofunguliwa soko lake ni duni.

Uvunaji

Vuna kunde zako baada ya kukomaa na kuanza kukauka kwa kung'oa mashina au kuchuma kwa mikono.Kisha zisambaze kunde zako au amshina yako juani ili zikauke zaidi na uweze kuziondoa kwa urahisi kutoka katika maganda yake.Unaweza kuondoa maganda uyake kwa mkono au kuupigapiga taratibu au kwa kutwanga katika kinu taratibu bila kuzipasua kunde.