FAHAMU KUHUSU KILIMO BORA CHA ALIZETI

Share:
Alizeti ni zao mojawapo la mafuta. Alizeti ni moja ya mazao yanayo vumilia ukame na hulimwa kwa ajili ya biashara na matumizi ya nyumbani.Mkulima anapotaka kupanda au kulima alizeti anapaswa kuzingatia yafuatayo ili kupata mavuno ya kutosha.


HALI YA HEWA NA UDONGO

Alizeti ni zao linalostahimili ukame na huwezwa kulimwa  kwenye maeneo yenye mvua  kidogo, wastani hadi mvua nyingi kiasi vilevile alizeti hufanya vizuri zaidi kwenye udongo wa tifutifu japo hufanya vizuri pia kwenye udongo wa mfinyanzi na kichanga.

KUANDAA SHAMBA

Mkulima wa alizeti anatakiwa/anashauriwa kutayarisha shamba  mapema kuanzia mwezi (Oktoba hadi desemba) kwa kukwatua ardhi na kulainisha vizuri udongo, mkulima lazima ahakikishe ameyavunja vunja vizuri mabonge  makubwa ya udongo shambani kabla ya kupanda, pia kama mkulima anaweza kupata mbolea ya samadi au mboji anaweza kuchanganya vizuri  samadi na udongo wakati wa kuandaa shamba.
Kuchanganya samadi kwenye udongo husaidia udongo kutunza maji kwa muda mrefu pia husaidia mizizi kukua vizuri (mizizi inakua haibanwi).
JINSI YA KUPANDA ALIZETI 
Upandaji wa alizeti hutegemea sana hali ya hewa ya eneo husika. Maeneo yenye mvua nyingi alizeti inatakiwa kupandwa mwishoni mwa mwezi Januari mpaka katikati ya mwezi Februari na Maeneo yenye mvua kidogo mfano mikoa ya Singida, Dodoma na Tabora alizeti hupandwa mwezi Desemba hadi Januari.

KIASI CHA MBEGU NA UPANDAJI WA ALIZETI

Kiasi cha kilo 4-5 za mbegu zinatosha kupanda eneo la ekari moja. 

Mkulima anashauriwa kupanda mbegu 2 – 3 katika kila shimo moja kwa nafasi ya sentimita 75 kutoka mstari hadi mstari na sentimita 30 kutoka shimo hadi shimo au sentimeta 75 kwa 40 au Sentimeta 90 kwa 30 kwa mbegu kubwa. Shimo la mbegu liwe na kina cha sentimita 3 – 5. 

Wiki mbili baada ya kuota, punguza miche katika kila shimo na kubakiza mche mmoja.


MBOLEA


Zao la alizeti ukilinganisha na mazao mengine ya nafaka na mbegu hufyonza virutubisho vilivyopo kwenye udongo  kwa kiwango kikubwa kutokana na alizeti kuwa na mizizi mingi. Hivyo kuongeza virutubisho kwenye udongo hufanya alizeti kukua vizuri na kutoa mazao mengi, hivyo mkulima anashauriwa kutumia mbolea stahiki na kwa wakati (wakati wa kupanda pia wakati wa kukuzia)
Wakati wa kupanda mkulima anatakiwa kutumia mbolea aina ya
  • DAP au NPK. mkulima anatakiwa kuweka gramu tano za mbolea (kifuniko kimoja cha soda ) katika shina wakati wa kupanda.
  • Baada ya kufanya palizi mkulima anashauriwa kuweka mbolea ya kukuzia. Alizeti hufanya vizuri kama itakuziwa na mbolea ya NPK kiasi cha gramu kumi (ganda moja la kiberiti ) katika shina moja.

KUZUIA MAGUGU




KUZUIA MAGUGU


Alizeti kama ilivyo kwa mazao mengine huathiriwa sana na magugu hasa alizeti inapokuwa bado ndogo hivyo kuondoa magugu ni jambo la muhimu na lazima. Alizeti inapokua kwenye shamba lisilokua na magugu hukua kwa haraka na kutengeneza kivuli kizuri( canopy) kinacho zuia magugu kuota. Kwa kawaida palizi inatakiwa kufanyika wiki mbili hadi tatu baada ya alizeti kuota.
Zipo njia mbalimbali za  kuzuia magugu kwenye alizeti. Mkulima anaweza kuondoa magugu katika shamba lake kwa kufanya yafuatayo;
  • Kuondoa magugu kwa kutumia jembe la mkono au kwa kuyang’oa kwa mikono
  • Kuondoa magugu kwa kutumia jembe la kukokotwa kwa ng’ombe au trekta maalumu
  • Kuondoa magugu kwa kutumia madawa ( viua gugu) maalumu vya kuondoa magugu shambani visivyo athiri alizeti.

MAGONJWA, WADUDU NA VIUMBE WANAOSHAMBULIA ALIZETI




MAGONJWA.

Alizeti hushambuliwa na magonjwa kadhaa yakiwemo:

Kuoza kwa mizizi, shina na kichwa

Hii husababishwa na kuwepo kwa hali ya unyevu kwenye udongo. Ugonjwa huu kusabaisha mimiea kuanguka shambani na huleta upotevu wa mazao

Madoa ya majani

Majani ya mmea ulioaathirika na ugonjwa huu huwa na mabaka ambayo husababisha mmea kushindwa kukua vizuri kutokana na kushindwa kutengeneza chakula kwenye majani

Kutu ya majani

Majani huwa na kutu, ugonjwa huu husababibisha mmea kushindwa kutengeneza chakula na hupelekea mmea kutoa mazao kidogo.

Kujikunja kwa majani

Ugonjwa huu husababishwa na virusi na kuenenzwa na nzi weupe pamoja na vidukari.
Mmea ulioshambuliwa huwa na dalili zifuatato; Kudumaa kwa mmea ulioshambuliwa, majani hupeteza rangi ya kijani kibichi na kuwa njano, kukunjamana kwa majani na kupungua ukubwa wa majani.

Ubwiri vinyoya (Downy Mildew)

Ugonjwa huu unasababishwa na kuvu (fangasi) na kuenezwa na mbegu, hewa na masalia ya alizeti. Unajitokeza wakati kuna unyevunyevu mwingi hewani hasa wakati wa Masika.
Dalili zake ni kama zifuatazo:
  • Madoa yenye umbo la yai, rangi ya njano iliyofifia hujitokeza kwenye majani makukuu na kusambaa mpaka kwenye majani machanga.
  • Baada ya siku chache madoa ya njano yanafunikwa na ukungu wa rangi ya kijivu.
  • Majani yanasinyaa na kufa kuanzia kwenye ncha.
  • Shina la mbegu huzungukwa na vidonda na kusababisha kichwa cha mbegu kuanguka.

Mnyauko wa vertisilia

Ugonjwa huu husababishwa na fangasi na huenezwa na masalia, maji yalio ambukizwa na hewa. Ugonjwa huu huonyesha dalili zifuatazo kwenye mazao;
  • Majani ya chini (majani yalio komaa) yanatengeneza mabaka mabaka kwa chini
  • Majani yanaanza kua ya njano kuanzia kwenye veini za jani na baadae huwa za rangi ya kahawia
  • Majani yalio athiriwa hukauka
  • Shina linabadilika rangi na kuwa na rangi nyeusi sehemu ya juu ya udongo
  • Ukipasua sehemu ya juu ya mmea inayo shikilia matawi/majani kwa ndani inakua na rangi nyeusi
Jinsi ya kukabiliana na magonjwa
  • Tumia mbegu safi na bora zilizothibishwa kitaalamu
  • Fanya kilimo cha mzunguko wa mazao, epuka kupanda zao moja kwa mfulizo katika shamba hilo ili kuzuia kuongezeka kwa vimelea wanaosababisha magonjwa
  • Vuna mazao mara tu yanapokomaa
  • Safisha shamba mara tu baada ya kuvuna ili kuzuia mazalia ya vimelea wanaosababisha magonjwa
  • Tumia dawa za kuua wadudu wanaoeneza magonjwa kama vile KARATE kwa kuua vidukari na nzi weupe wanaoeneza ugonjwa unaosababishwa na virusi.
  • Kama mimea iliyo athirika ni michache shambani, ng`oa mimea yote inayoanza kuonesha dalili za ugonjwa ili kuzuia uginjwa kuendelea kusambaa kwenye mimea ambayo haijaathirika shambani. Kisha pulizia dawa ya kuua wadudu

WADUDU NA WANYAMA WANAOSHAMBULIA ZAO LA ALIZETI

Zao la alizeti hupendelewa sana na wadudu kutokana na kuwa na maua makubwa na yenye rangi nzuri inatovutia wadudu, ndege na hata wanyama. Baadhi za wadudu hupendelea kutua kwenye zao hili bila kusababisha uharibifu, mfano nyuki na vipepeo ambao hufanya uchavushaji. Viumbe waharibifu wa zao hili ni pamoja na:

Ndege (kwerea kwerea)




Hawa ndio viumbe waharibifu zaidi wa zao hili. Alizeti hushambuliwa sana na ndege ambao huweza kusababisha upotevu wa zaidi ya 50% ya mazao

Namna ya kukabiliana na ndege

  • Fyeka vichaka vyote vilivyo karibu na shamba ambavyo ndio vituo vya ndege
  • Epuka kupanda alizeti karibu na miti au misitu
  • Vuna mapema mazao mara tu baada ya suke kukomaa
  • Weka sanamu au vitu vitavyoweza kuwatisha ndege katika shamba la alizeti
Funza wa vitumba (American ballworm)

Mdudu huyu ni hatari sana kwa mazao mengi ikiwemo alizeti. Hushambulia zao hili kwa kukata mimea ikiwa michanga, mara tu vitumba vya maua vinapoanza na kipindi chote mpaka zinapokaribia kukomaa

Jinsi ya kukabiliana na funza

  • Tumia dawa yoyote ya kuua wadudu mfano KARATE
  • Fanya kilimo cha mzunguko wa mazao kuzuia mazalia ya wadudu katika shamba
  • Kusanya na kuchoma moto au kufukia mabaki yote ya mazao shambani baada ya kuvuna
  • Haribu mazalia yote ya vipepeo kwenye vichaka karibu na shamba ili kuzia wadudu kuendelea kuzaliana kipindi ambacho zao halipo shambani

UVUNAJI WA ALIZETI     


DALILI ZA KUKOMAA


Uvunaji wa Alizeti unapaswa ufanyike endapo zaidi ya asilimia 80 ya mbegu zilizopo kwenye ua/suke zimebadilika rangi na kuwa ya nyeusi au Kahawia ili kupunguza upotevu unaoweza kusababisha na ndege  na kuvunjika kwa mmea na kuanguka. Pia wakati wa kuvuna majani yanabadilika rangi na kuwa rangi ya njano.
Pia mmea wa alizeti unakua umekomaa endapo nyuma ya ua/suke kunabadilika rangi kutoka rangi ya kijani na kua ya njano na kikonyo hubadilika na kua rangi kahawia. Hii hutokea katika siku ya 30 hadi 45 baada ya suke ya alizeti kuchanua. Kwa ujumla mmea wa alizeti hukomaa siku ya 125- 130 baada ya kuotesha.

 NJIA ZA UVUNAJI

Alizeti huvunwa kwa kukata ua (masuke) kwa kutumia vifaa vyenye makali kama kisu au mundu. Baada ya kukata masuke huanikwa kwenye maturubai ili kuhakikisha unyevunyevyu umepungua kwa kiasi kikubwa kutoka kwenye mmea kabla ya kupuchukua. Mbegu za alizeti hupukuchuliwa kwa kuyapigapiga ili zitoke kwenye suke.
Pia ipo njia ya kutumia mashine maalimu (Combines) ambayo hukata mmea, kutenganisha mbegu kutoka kwenye ua, kuondoa takataka zilizopo kwenye mbegu na kusafirisha mbegu kwa ajili ya kuhifadhi.

MBINU BORA ZA KUTUNZA ALIZETI BAADA YA KUVUNA


KUCHAMBUA


Baada ya kuvuna alizeti, uchafu wa aina yoyote uliojichanganya na mbegu za alizeti mfano: mawe, mbegu za magugu, majani n.k hupaswa kuondolewa na pia mbegu za alizeti zinapaswa kutenganishwa na kuwekwa katika mafungu kulingana na rangi na ukubwa wa mbegu ili kukidhi vigezo na mahitaji ya soko.

KUFUNGASHA

Mbegu za Alizeti zinapaswa kuwekwa katika vifaa maalumu visivyoruhusu wadudu wala unyevunyevu kuingia kama vile mifuko maalumu kulingana na rangi na ukubwa wa mbegu.

KUHIFADHI

Endapo mbegu ya alizeti itahifadhiwa kwa muda mfupi, kiwango cha unyevunyevu kinachotakiwa kiwepo kwenye mbegu ni chini ya asilimia 12 na endapo itahifadhiwa kwa muda mrefu kiwango cha unyevunyevu unaohitajika ni chini ya aslimia 10. Mbegu zikiwa kwenye vifungashio maalumu zinapaswa kuhifadhiwa kwenye ghala/chumba maalum.
Ghala la kuhifadhia linapaswa kuwa na sifa zifuatazo:
  • Liwe na hewa safi inayopita ili kuzuia kuibuka kwa magojwa yatokanayo na hewa chafu.
  • Liwe limeezekwa vizuri ili kuzuia paa kuvuja na kuharibu mazao wakati wa mvua.
  • Lisiwe na mianya ya kuruhusu wadudu kuingia kwasababu wadudu waharibifu wanaweza kuharibu mazao.
Mbegu za alizeti zinaweza zikahifadhiwa kwa zaidi ya msimu mmoja lakini kitaalamu haishauriwi kuifadhi zaidi ya msimu mmoja ili kuzuia kupungua kwa ubora.