Mbinu Bora za Kilimo cha Matunda ya Pesheni

Share:

Pesheni ni aina ya tunda, kitaalamu Passiflora edulis ni mmea wa kudumu unaotambaa na unaokua katika maeneo ya tropiki na nusu-tropiki unaozaa matunda ya ukubwa wa yai yaliyo ya rangi ya Njano au Zambarau yenye kunukia vizuri. Mmea huu hukua katika maeneo ya joto mpaka ya baridi kiasi, altitudi ya mpaka mita 2000 juu ya usawa wa bahari, katika kiwango cha wastani cha mvua/unyevu na udongo wa wastani mchanganyiko kichanga na kifinyanzi.

Aina za Pesheni:
Pesheni ya rangi ya Njano
hutoa matunda makubwa zaidi na hata mashina yake ni makubwa zaidi, pia aina ya Njano hupendelea na hukua vizuri katika maeneo ya mwinuko wa chini na joto (tropiki), aina hii ya njano ambayo huanza kuzaa miezi 12 baada ya kupandwa na huzaa kwa wingi sana

Pesheni ya rangi ya dhambarau
huwa madogo zaidi yenye uchachu kidogo, utamu, juisi nyingi na hunukia zaidi. pesheni ya Zambarau hupendelea mwinuko kiasi mpaka wa juu takribani mita 2000 na hali ya baridi kiasi. Aina ya Zambarau hukua haraka na huzaa miezi 7 mpaka 9 baada ya kupandwa shambani na huwa na vipindi viwili vya mavuno ya juu kwa mwaka hasa miezi ya Julai na Januari

Uzalishaji na Mpangilio wa Shamba:
Pesheni huzalishwa kwa kutumia mbegu. Chagua matunda bora yaliyokomaa na kuiva vizuri kisha ondoa mbegu. 

Panda mbegu katika tuta lililoandaliwa vizuri au kwenye viriba/mifuko iliyojazwa udongo uliochanganywa na mchanga kidogo na mbolea ya samadi. 

Mbegu huota na kuchipua wiki 2 mpaka 3 baada ya kupandwa. Mbegu zilizohifadhiwa muda mrefu huchelewa kuota na uotaji wake huwa wa chini. Miche hupandikizwa shambani ikifikia kimo cha sentimita 25 mpaka 30.

Mashimo yachimbwe yenye ukubwa wa sentimita 50 urefu, upana na kimo, yakiachana mita 2 mpaka 4 katika mstari na mita 3 mpaka 4 baina ya mstari na mstari kutegemeana na matumizi ya ardhi kwa mkulima mwenyewe. 

Panda miche katika mashimo yenye udongo uliochanganywa na samadi au mboji vizuri, waweza pia kuongeza mbolea ya chumvichumvi ya kupandia na kukuzia. 

Chimbia nguzo urefu wa wastani mita 2 juu ya ardhi kufuata mistari zikipishana mita 6 mpaka 9 na unganisha kwa waya au kamba imara. Nguzo zaweza kuwa za chuma au mti kulingana na uwezo wa mkulima mwenyewe.

Miche inapokua ielekeze vizuri kwa kuishikiza kuelekea juu kuushika waya/kamba ya juu ili itambae nao vizuri. 

Hakikisha shamba lako linasafishwa vizuri na kuepuka magugu. Waweza kuchanganya mazao ya muda mfupi kama mbogamboga na mikundekunde katikati ya mistari ya Pesheni ili kutumia ardhi vizuri .

Kuvuna:
Matunda yaliyokomaa na kuiva huanguka chini yenyewe, hivyo wakati wa mavuno kumbuka kupita kuokota muda wa asubuhi kila siku. 

Mavuno kwa mwaka katika shamba lililotunzwa vizuri huwa kati ya tani 9 mpaka 15 kwa hekta, hivyo kwa nusu hekta (mita 50 urefu kwa 50 upana) utapata kati ya tani 4.5 mpaka 7.5.

Muda wa Kuhifadhi rafuni (shelf life):
Matunda yanaweza kuhifadhiwa vizuri katika sehemu yenye kivuli, hewa inayozunguka vizuri na joto la kawaida kwa wiki 1 mpaka 2, waweza pia kuhifadhi kwa wiki 4 mpaka 5 katika nyuzi joto 7, ila zingatia baridi ikizidi sana yaweza kusababisha mashambulio ya fangasi.