MBINU BORA ZA KILIMO CHA PILIPILI HOHO

Share:

MATUNZO YA SHAMBA
Matunzo ya shamba ni muhimu sana kwa sababu huamua kiasi cha mavuno unayoweza kupata kutoka shambani. Shamba ambalo halipati matunzo mazuri hata kama mbegu bora inayozaa sana itatumika mavuno bado yatakuwa hafifu. Matunzo ya shamba hujumuisha.
Umwagiliaji
Njia za umwagiliaji
Kuna njia tofauti za umwagiliaji ambazo zinaweza kutumika katika umwagiliaji wa bustani ya pilipili hoho kama vile umwagiliaji wa njia ya matone (drip irrigation), wa njia ya mifereji na umwagiliaji wa kutumia cane. Kwa kilimo cha kiangazi au pale mvua zinapokuwa hafifu ni muhimu kufanya umwagiliaji wa bustani yako ili kuepuka kunyauka kwa mazao shambani kutokana na upotevu mkubwa wa maji. Wakati wa kumwagilia hakikisha haumwagii maji katika majani bali katika shimo chini ya kichaka cha mche (canopy).
 Ratiba ya umwagiliaji
Kwa kipindi cha kiangazi ni muhimu kuwa na ratiba moja ya umwagiliaji wa bustani. Unaweza kumwagilia bustani yako kila baada siku mbili hadi tatu kutegemeana na hali ya hewa na udongo. Cha msingi usiache udongo ukauke bali mwagia maji angalau asilimia hamsini ya unyevu wa udongo unapokuwa umepotea. 
Mambo ya kuzingatia
Ni vyema umwagiliaji wa bustani uzingatie hatua za ukuaji wa mimea bustanini, hali ya hewa na uwezo wa udongo kutunza maji. Mahitaji ya maji kwa pilipili hoho huongezeka wakati wa kutoa maua na kutengeneza matunda. Vilevile katika maeneo yenye hali ya joto na udongo wa kichanga maji hupotea kwa urahisi. Hakikisha maji hayatuami katika shamba lako kuepuka kuoza kwa mizizi na udongo haukauki.
Kuweka Mbolea
Zao la pilipili hoho huitaji sana virutubisho vya Naitrojeni (nitrojen), fosfati (phosphorus), potashi (potassium) na chokaa (calcium). Virutubisho vingine ni pamoja na magnesium, Sulphur, zinc na boron.
Mbolea ya kukuzia
Weka mbolea ya kukuzia aina ya CAN majuma mawili hadi matatu tangu kupandikiza kwa kiwango cha kizibo kimoja cha soda kuzunguka shina. Mifuko miwili ya kilo 50 inaweza kutumika katika eneo la ekari moja. Vile vile inashauriwa kuweka mbolea ya mchanganyiko (N.P.K.) wakati maua yanapoanza kutoka. Waweza kutumia N.P.K ya maji kunyunyizia majani kila baada ya wiki mbili tangu kutoka kwa maua.
Kuweka Matandazo
Matandazo husaidia kudhibiti magugu, kuifadhi unyevu na kuongeza rutuba katika udongo. Kwa matokeo mazuri katika udhibiti wa magugu inashauriwa kuweka matandazo kwa kuyatandaza katika udongo katika kina cha sm 10 mpaka 15 maeneo yote ya tuta kuzunguka mashimo ya miche. Matandazo ya asili kama mabua ya nafaka, pumba za mpunga, maganda ya karanga na maranda ya mbao yanaweza kuwekwa kabla ya kupandikiza baada ya kuchimba mashimo ya kupandia au baada ya kupandikiza. Matandazo ya plastiki huwekwa mapema kabla ya kupandikiza baada ya kuandaa matuta.
Kusimikia miti (staking)
Mmea wa pilipili hoho kama ilivyo kwa zao la nyanya huitaji kusimikwa miti ili zisianguke kutokana na mzigo wa matunda na upepo. Simika miti katika bustani ya pilipili hoho wiki tatu tangu kupandikiza hasa baada ya kutoka kwa ua la kwanza. Simika miti yenye urefu wa m 1.5 hadi mita 2  pembeni ya kila mmea umbali wa sm 5 kutoka kwenye usawa wa majani na kufunga kwa kamba shina la mmea na mti  kwa kifundo chenye umbo la namba nane. Hakikisha unatumia miti imara isiyooza kwa haraka yenye unene usiopungua sentimita 2.
Kupogolea
Katika mmea wa pilipili hoho upogoleaji hufanyika kwa kundoa majani yaliyo zidi na yaliyo athirika na magonjwa ili kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa katika mmea. Kwa mbegu chotara zinazo zaa kwa muda mrefu pogolea matawi na majani baada ya kuvuna katika kila ngazi ili kuruhusu utengenezwaji mzuri wa matunda kwa ngazi ya juu yake. Vilevile inashauriwa kukata ncha ya shina baada ya kutokea kwa ngazi tano au sita katika mmea ili kuzuia ukuwaji wa mmea kwenda juu na kuchochea ukuwaji mzuri wa matunda. Ondoa ua la kwanza la pilipili hoho kuchochea utokaji wa maua na matunda mengi. Epuka upogoleaji uliokithiri kwani huweza kusababisha hitilafu ya kuungua kwa matunda ya pilipili hoho kutokana na mwanga wa jua.
KUVUNA
Kiwango cha mavuno
Kiwango cha mavuno ya pilipili hoho kwa ekari moja hutegemeana na matunzo ya shamba, uwezo wa kuzaa wa mbegu iliyotumika na idadi ya mimea katika shamba.   Mbegu za aina tofauti zina uwezo tofauti wa kuzaa na hivyo mavuno huwa tofauti. Vilevile mashamba tofauti yaliyopandwa mbegu ya aina moja na kupata matunzo ya viwango tofauti huwa na kiwango tofauti cha mavuno. Kwa wastani mmea mmoja wa mbegu bora (chotara) uliotunzwa vizuri una uwezo wa kutoa karibu kilo 3 mpaka 5 za pilipili hoho.
Muda wa Kuvuna
Pilipili hoho huwa tayari kuvunwa baada ya miezi miwili na nusu hadi mitatu tangu kupandikiza miche. Muda wa kuvuna hutegemeana na matumizi ya pilipili hoho ambapo kwa matumizi ya nyumbani huvunwa zikiwa zimekomaa, ngumu na zenye rangi ya kijani kibichi inayong’aa. Kwa ajili ya kusindika kiwandani huvunwa zikiwa zimekomaa na zenye rangi ya njano au nyekundu kutegemeana na aina ya mbegu iliyotumika. Uvunaji huweza kuendelea kwa muda wa miezi miwili hadi mitatu ukiendelea kuhudumia bustani vizuri. Kwa kilimo cha ndani ya nyumba kitalu (greenhouse) huvunaji huendelea kwa muda wa hadi miezi sita.