Nyanya Chungu ni zao la Kitropic linalotoa mazao yake kama matunda au kama mboga. Rangi ya matunda huwa kijani kibichi au kijani-njano, au njano-nyupe. Kuna aina mbalimbali za nyanya chungu ambazo ni ni nyanya chungu za asili na zingine ni chotara siyo chungu kama za asili.
MAZINGIRA
Zao hili hustawi vizuri maeneo yenye baridi ya wastani na joto la wastani kuanzia nyuzi joto 25°C hadi 35°C, hupendelea udongo tifu tifu usiotwamisha maji na wenye rutuba. Kama utaweza kutumia mbolea za samadi na mboji au mbolea za asili pamoja , basi nyanya chungu hustawi vizuri sana.
KUANDAA KITALU
Mbegu za nyanya chungu huandaliwa kwenye kitalu kwanza kabla ya kupelekwa shambani.
Maelekezo ya kuandaa kitalu cha nyanya chungu.
- Chagua eneo la kuanzisha kitalu kwenye maeneo yanayopatikana maji kwa urahisi.
- Inua udongo wa kitalu hadi kufikia kimo cha sm 20 na upana wa mita 1 na urefu wowote. Bonda bonda mabonge makubwa ya udongo ili kupata udongo laini.
- Weka mbolea ya asili iliyooza vizuri, changanya ndoo moja kubwa ya lita 20 ya mbolea hiyo kwa eneo la mita 1 kwa mita 1 (1 m2). Kwa hiyo kama tuta lako la kitalu lina urefu wa mita 5 na upana mita 1, utaweka ndoo 5 za mbolea za asili.
- Kama ni wakati wa kiangazi, mwagilia tuta lako kwa siku 3 mfululizo mpaka udongo uloane vizuri.
KUSIA MBEGU
Maelekezo ya namna ya kusia mbegu kwa usahihi
- Tengeneza vimifereji vyenye kina cha sm 2 kukatisha tuta, nafasi kati kimfereji kimoja na kingine ni sm 15 au nusu rula.
- Sia mbegu zako ndani ya vimifereji hivyo, halafu funika na udongo laini.
- Weka matandazo ya nyasi juu ya tuta ili kuzuia jua kali na matone ya maji ya moja kwa moja.
- Mwagilia maji kitalu chako juu ya nyasi asubuhi na jioni kila siku. Ila inashauriwa kumwagilia kitalu chako maji wakati wa jioni.
- Mbegu za nyanya chungu huota baada ya siku 10 hadi 14 tangu kusia. Baada ya mbegu kuota toa matandazo ya nyasi halafu yaweke matandazo hayo katikati ya mistari ya miche.
- Tengeneza kivuli cha matandazo ya nyasi juu ya kitalu chenye kimo cha mita moja, kivuli hicho cha nyasi lazima kiwe kinapitisha mwanga wa jua walau kidogo ili kuruhusu mwanga kuifikia miche.
KUPANDIKIZA MICHE SHAMBANI
Miche huwa tayari kuhamishiwa shambani baada ya mwezi mmoja hadi mwezi mmoja na nusu tangu mbegu kuota. Nafasi ya kupandikiza nyanya chungu ni mita 1 kwa mita 1 (yaani mita 1 shina hadi shina na mita 1 mstari hadi mstari)
Kabla ya kupandikiza miche chimba mashimo yenye ukubwa kiasi, weka samadi iliyooza vizuri kiasi cha mkono mmoja uliojaa, halafu fukia udongo kiasi. Baada ya kufukia udongo pandikiza mche wako, kila shimo mche mmoja. Kama ni kipindi cha kiangazi pandikiza wakati wa jioni, baada ya kupandikiza mwagili maji vizuri.
KUTUNZA SHAMBA
Mimea jamii ya mbogamboga ikiwemo nyanya chungu haipendi bugudha ya magugu shambani, kwa hiyo hakikisha unafanya palizi wakati wote kuakikisha magugu hayaathiri ustawi wa mmea.
Dhibiti magonjwa na wadudu mabalimbali wanaoathiri zao hili, kwa kutumia madawa mabalimbali na matumizi ya mbolea mbalimbali za kurutubisha mimea pale inapobidi na iwe ya kilimo hai.
KUVUNA
Nyanya chungu huwa tayari kuvunwa ndani ya siku 90 hadi 120 tangu kupandikiza. nyanya chungu inaweza kuvunwa mara 1 au mara 2 kwa wiki. Matunda ya nyanya chungu yanatakiwa kuvunwa kabla hayajabadilika rangi kutoka nyeupe kwenda njano mpauko.
matunda haya ya nyanya chungu yanaweza kusindikwa kuwa unga. Ili kusindika nyanya chungu kuwa unga fwata hatua zifuatazo;
- Chagua nyanya chungu bora na zioshe kwenye maji
- Kata kata nyanya chungu hizo kutengeneza vipande vidogo dogo, halafu tandaza vipande hivyo kwenye mkeka au turubai safi
- Anika vipande hivyo vya nyanya chungu juani hadi vikauke.
- Baada ya vipande hivyo kukauka vizuri, visage kwa kutumia kinu au mashine ya mkono mpaka viwe unga.
- Tunza unga huo kwenye chombo kisafi ambacho hakingizi hewa.
- Unaweza kutumia unga huo kwenye maharage, karanga, nyama na mboga zingine, mboga iliyowekwa unga huu wa nyanya chungu inakua tamu mno na inakua na virutubisho vya kutosha.