KILIMO CHA MCHICHA (AMARANTH)

Share:
Mchicha ni aina mojawapo ya mboga za majani ambayo hulimwa sehemu nyingi za Tanzania. Mbegu na majani yake yana vitamini A, C, madini ya aina ya chokaa na chuma kwa wingi. Majani ya mchicha hutumika kwa mboga na mbegu zake zinaweza kusagwa na unga wake kutayarishwa chakula cha mtoto au huchanganywa na unga wa aina nyingine kama vile ngano, mahindi, mtama kwa ajili ya vitafunio.

AINA YA MCHICHA
- Mchicha mweupe ambao una majani membamba yenye rangi ya kijani isyokolea. Mchicha huu huvunwa kwa njia ya kung'oa;

- Mchicha mpana ambao una majani mapana yenye rangi ya kijani iliyokolea;

- Mchicha mwembamba wenye rangi mchanganyiko wa zambarau na kijani ambao huota wenyewe shambani kama magugu;

- Mchicha mwekundu ambao una majani mekundu;

- Mchicha pori ambao una rangi ya kijani ambao ukishakomaa unatoa miiba.

UDONGO
Mchicha hustawi kwenye udongo wowote wenye utuba ambao hausimamishi maji.

KUTAYARISHA BUSTANI
Tayarisha bustani kwa kufyeka majani, lima na tifua ardhi mwezi mmoja kabla ya kupanda. Weka mbolea ya samadi ya kuku au mboji ili kuongeza rutuba. Tumia debe moja la mbolea katika eneo la mita moja za mraba. Changanya vizuri udongo na mbolea kisha sawazisha.

KUPANDA
Mbegu za mchicha zinaweza kupandwa moja kwa moja bustanini kwa kutawanya au kupanda kufuata mstari. Baadaye miche inaweza kupunguzwa ili kuipa miche iliyobakia nafasi ya kukua vizuri.

Njia nyingine ya kupanda mchicha ni ile ya kuotesha mbegu kwenye kitalu na baadaye kuhamishia kwenye bustani. Mbegu hizi zinaoteshwa kwenye tuta kwa njia ya kusia kufuata mstari. Aina za mchicha ambazo zinafaa kuoteshwa kwenye kitalu ni ile yenye mbegu nyeupe na majani mapana.

KUHAMISHA MICHE
Miche ya mchicha inakuwa tayari kuhamishiwa kwenye bustani baada ya wiki mbili. Siku moja kabla ya kuhamisha, miche imwagiliwe maji ili kurahisisha ung'oaji wake.

Wakati wa kupandikiza miche ipandikizwe katika nafasi zifuatazo:
- Aina fupi za mchicha, miche ipandwe katika nafasi ya sentimita 15 hadi 22 toka shimo hadi shimo na sentimita 28 hadi 30 kati ya mstari na mstari;

- Aina ndefu za mchicha, miche ipandikizwe katika nafasi ya sentimita 60 kati ya mche na mche na sentimita 60 kati ya mstari na mstari.

KUTUNZA BUSTANI
Palizi
- Ni muhimu kupalilia bustani ili kuondoa magugu.

Umwagiliaji
Vile vile bustani imwagiliwe maji kila siku asubuhi na jioni, hasa wakati miche bado  michanga.

Mbolea
Tumia mbolea ya kuku kwa ajili ya kukuzia miche ya mchicha.

Magonjwa na wadudu waharibifu
Mchicha hushambuliwa zaidi na ugonjwa wa kinyeusi. Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hushambulia miche michanga kwenye shina usawa wa ardhi. Shina lililoshambuliwa hukauka na hatimaye mmea wote hunyauka na kukauka.

Wadudu ambao hushambulia mchicha ni pamoja na utitiri, vidukari, mbawakau, na kinyambisi au kinyafungo.

Utitiri
- Hawa ni wadudu wadogo sana wenye rangi ya machungwa, nyekundu au kahawia. Wadudu hawa huishi chini ya jani na kufyonza utomvu wake. Jani lililoshambulliwa hugeuka rangi na kuwa manjano, husinyaa, hujikunja na hatimaye kunyauka.

Vidukari
Hawa pia ni wadudu wadogo wenye rangi ya kijani, nyeusi au kahawia ambao hushambulia miche kwa kunyonya utomvu wake. Miche hudhoofu, huduma na hatimaye hufa.

Mbwakau
Viwavi wa mbwawakau hushambulia majani ya mchicha.

Kinyambisi na kinyafungo
Huyu ni mdudu mwenye rangi ya kijani kibichi na ana harufu mbaya. Mdudu huyu hushambulia mbegu changa za mchicha kwa kufyonza utomvu wake hadi mbegu zinabakia makapi matupu.

KUVUNA
Mchicha uko tayari kwa kuvunwa baada ya wiki mbili hadi nne tangu kupandwa. Mchicha unaweza kuvunwa kwa kung'oa au kwa kukata majani ya juu na kuacha mashina yaendelee kuchipua. Katika hali hii bustani iendelee kuchipua. Katika hali hii bustani iendelee kumwagiliwa maji.

Mchicha uliotunzwa vizuri unaweza kuendelea kuvunwa kwa miezi mitatu au zaidi. Hata hivyo mchicha wa mbegu uvunwe baada ya mbegu kukomaa kisha ukaushwe juani ili kupata mbegu.