Katika warsha nyingi ambazo taasisi tofauti tofauti zilizofanyika na wakulima, dhana hili imejadiliwa kwa kiasi kikubwa.
Baadhi ya majibu yaliyotolewa na wakulima juu ya maana ya mazingira ni pamoja na;
- Kupanda miti
- Wanyama wengi wa porini
- Kuweka safi maeneo ya nyumbani
- Vitu vyote vinavyo tuzunguka
- Kuchimba makingamaji
- Mambo yote yanayo tuzunguka
- Ni misitu
- Shamba lililo bora na kadhalika.
Ukiangalia majibu hayo utaona kuwa kila, mmoja alikuwa anaelewa mazingira kwa namna yake. Watu walisahau kuwa hata vitu visivyo hai kama mawe in mojawapo ya mazingira. Pia hata vile visivyoonekana kwa macho yetu pia ni sehemu ya mazingira.
Baada ya majadiliano marefu kwa pamoja wote wanakubaliana kuwa Mazingira ni:
Jumla ya vitu vyote vavyotuzunguka sisi binadamu, vilivyo hai na visivyo hai, vya karibu na mbali, vinavyoonekana.
Vyote hivi vipo ama juu angani, chini ya ardhi au kwenye uso wa ardhi. Mifano michache ni kama ardhi yenyewe, miti, wanyama, mawe, mito, maziwa, bahari, mimea, wadudu, hewa (haionekani) mawimbi ya redio (hayaonekani) hata nguo tulizovaa.
Hapo ulipo sasa hivi angalia vitu vyote vinavyokuzunguka na ndiyo vinavyounda mazingira yako kuanzia vya karibu kama nguo na vile vya mbali kama jua.
Ni vizuri kuyajua mazingira yako ili uweze kuyatumia vizuri na kuchukua tahadhali kwa yale mabaya yaliyomo ndani yake kwa uendelevu.
Hata vitabu vya dini vinasema tukikabidhiwa ulimwengu na vitu vyake vyote ili tukavitawale. Hivyo ukiyatawala mazingira utaishi kwa aha, ukiacha yakutawale wewe, utaishi kwa taabu. Ardhi na mazingira vimeharibika kutokana na matumizi yasiyo endelevu. Mfano kukata miti ovyo kumeleta ukame na matatizo mengi. Kufuga mifugo mingi kuliko uwezo wa eneo pia kumeeneza jangwa n.k. Majanga mengine ni asili hatuna uwezo nayo ingawa tahadhali zinatakiwa kuchukuliwa pia. Majanga hayo ni kama ukame, mafuriko namatetemeko.