KILIMO CHA MUHOGO

Share:
Muhogo ni zao lenye uwezo wa kustahimili ukame hivyo linaweza kulimwa hat sehemu zenye mvua chache. Hustawi vizuri zaidi katika sehemu zenye joto. Sehemu za baridi zao hili juchelewa sana kukomaa na pengine kushindwa kabisa kustawi.

Muhogo huhitaji udongo tifutifu au wa kichanga kiasi na wenye rutuba ya wastani. Udongo mzito unaotuamisha maji haufai kwa kilimo cha muhogo. Muhogo licha ya kuwa chakula cha binadamu, una matumizi mengi. Majnai yake machanga hutumika kama mboga ijulikanayo kwa jina la kimsamvu. Majani haya yana vitamini A kwa wingi.

KUTAYARISHA SHAMBA
Shamba halina budi litayarishwe mapema. Hivyo tayarisha shamba mwezi mmoja au miwili kabla ya mvua za mwanzo. Kata miti, fyeka vichaka na ng'oa visiki vyote, kusanya na choma moto nje ya shamba. Kisha lima ardhi, tifua na lainisha udongo. Kama utapanda muhogo katika matuta, tengeneza matuta yaliyoinuliwa kidogo kiasi cha sentimita 60 - 90. Nafasi kati ya tuta na tuta iwe sentimita 150.

KUPANDA
Muhogo hupandwa kwa kutumia pingili. Pingili hizi zinatakiwa ziwe na urefu wa sentimita 25 hadi 30. Sehemu ya katikati ya shina ndiyo inayofaa kukatwa pingili. Sehemu ya juu haifai kwa vile ni changa.

Panda mara mvua zinapoanza kunyesha. Panda kwa kufukia sehemu kubwa ya pingili ardhini na kuzilaza msharazi kidogo. Kwa migo inayopandwa katika sesa tumia nafasi ya sentimita 120 kati ya mstari na sentimita 90 toka mmea hadi mmea. Ikiwa utapanda katika matuta, panda katika nafasi ya senytimita 150 kati ya mstari na mstari na sentimita 75 kati ya shimo na shimo.

KUTUNZA SHAMBA
Palizi
Magugu ni moja ya maadui wakubwa wa muhogo, hivyo palizi ni muhimu sana. Ili kupata mavuno mengi na bora. Shamba halina budi lipaliliwe mara tatu. Palizi ya kwanza ianze mwezi mmoja tangu kupanda na zingine zifuate kila baada ya mwezi mmoja kutegemea na utoaji wa magugu. Palizi ifanyike kwa uangalifu ili kuepuka kukata mizizi ya mihogo. Wakati wa kupalilia rudishia udongo kwenye mashina.

Magonjwa
Muhogo hushambuliwa na magonjwa ya aina nyingi kama haya yafuatayo:-

Batobato (Cassava mosaic)
Ugonjwa huu hushambulia majini na hunezwa na inzi weupe. Majani yaliyoshambuliwa hujikunja na huwa na mabaka mabaka ya kijani na manjano. Baadaye mmea hudumaa na majani hupukutika. Zuia ugonjwa huu kwa kupanda aina za muhogo zinazostahimili ugonjwa huu; kwa mfano aina ya Kibaha, Msitu, Zanzibar, Mzimbitala na Kigoma. Pia epuka kupanda pingili zilizotoka kwenye muhogo ulioshambuliwa na ugonjwa huu na ikiwezekana ng'oa muhogo wote ulioshambuliwa na choma moto.

Mabaka ya kahawia
Ugonjwa huu hushambulia shina, majani na mizizi. Shina na majani hupata mabaka ya rangi ya manjano. Mizizi hupinda na huwa na vidonda; na ikikatwa madoa meusi au kahawia hunekana. Zuia ugonjwa huu kwa kutumia mbegu bora ambazo hazikushambuliwa na ugonjwa huu na ing'oe mihogo iliyoshambuliwa na ichom.

Wadudu Waharibifu
Vidugamba (Scales)
Ni wadudu wadogo weupe wanaonekana kama magamba kwenye shina na matawi ya muhogo. Wadudu hawa hufyonza utomvu wa mmea na usababisha mmea udumae, majani yake kuwa na rangi ya manjano na hatimaye kupukutika. Mashambulizi yakizidi mmea hukauka.

Kuzuia
- Panda pingili zisizokuwa na wadudu hawa. Pia kabla ya kupanda, pingili zichomwe kwenye dawa ya kuzuia wadudu hawa. Dawa hizi ni kama vile Fenitrothion 50% na Diazonon 60% E.C.

Buibui wa muhogo (cassava spidermites)
Wadudu hawa ni wadogo na wana rangi ya kijani. Hufyonza utomvu wa majini machanga. Majani yaliyoshambuliwa huwa na madoa ya rangi ya manjano na nyeupe. Hukunjamana na hatimaye hunyauka na kupukutika kuanzia nchani. Zuia wadudu hawa kwa kupanda pingili ambazo hazina wadudu hawa. Panda aina za muhogo zinazostahimili nashambulizi ya wadudu hawa. Aina hizi ni kama vile mzimbitala na kanyamzige.

Mchwa
Mchwa hushambulia pingili zilizopandwa. Ili kuepukana na tatizo la mchwa panda mapema na tumia dawa aina ya Alandrin 40% W.P. changanya gramu za dawa kwenye lita 20 za maji, halafu nyunyiza kwenye pingili na shimo la kupandia.

Vidungata (Cassava mearly bugs)
Wadudu hawa wana umbo la yai na rangi ya pinki. Miili yao imefunikwa na vumbi jeupe mfano wa unga. Vumbi hili hunata kidogo. Vudangata hufyonza utomvu wa mmea na husababisha majani kuanguka, pingili kuwa fupi na kupinda. Mashambulizi yakizidi mmea hufa kuanzia nchani.

Kuzuia
- Panda aina ya muhogo inayostahimili;
- Usisafirishe pingili au kisamvu kutoka eneo lenye wadudu hawa kupeleka sehemu nyingine;
- Tumia wadudu jamii ya manyigu;
- Kama mashambulizi ni makubwa ng'oa muhongo na choma moto.

Wanyama waharibifu
Baadhi ya wanyama waharibifu wa muhogo ni panya, fuko, nguruwe, nyani na ngedere. Wadhibiti wanyama hawa kwa kuweka mitego au kuwawinda. Pia panda aina chungu za muhogo kama vile kimbaga na mbwana. Panda mihogo hii kuzunguka shamba la mihogo.

KUVUNA NA HIFADHI
Vuna majani ya muhogo yakiwa bado machanga ili kupata kisamvu kizuri. Kisamvu kinaweza kutayarishwa kwa kutwangwa na kupikwa moja kwa moja au kukaushwa baada ya kutwangwa kwa matumizi ya baadaye. Twanga kisamvu katika kinu hadi kilainike. Weka kwenye sufuria na maji kiasi, bandika kwenye moto na upike kama mboga zingine.

Twanga kisamvu katika kinu hadi kilainike. Kisha kitoe na kukifunga kwenye nailoni au kitambaa. Tumbukiza kisamvu kiwe na rangi yake ya asili, kupunguza muda wa kupika baada ya kukaushwa na kuzia vijidudu vingine viharibifu. Hakikisha kuwa sehemu zote zinapikwa. Kitambaa kitolewe na kutumbukizwa ndani ya maji baridi ili kisamvu kisipikike zaidi. Tandaza mboga baada ya siku moja hadi mbili. Hifadhi mboga zako katika mifuko ya nailoni, tayari kwa matumizi ya baadaye.